Friday, March 8, 2013

VIFO VINGI VYA KINAMAMA WAJAWAZITO VINATOKANA NA KUCHELEWA KUFIKA HOSPITALINI

                                                                                          Na Anna Nkinda – Mwanza

Imeelezwa kuwa kutokana na tatizo la baadhi ya kina mama wajawazito kuchelewa kufika Hospitali mapema kujifungua wengi wao wanakufa kutokana na tatizo la kupasuka kwa mfuko wa uzazi, kutokwa na damu nyingi kabla na baada ya kujifungua na kifafa cha mimba.

Hayo yamesemwa jana na Daktari wa Mkoa wa Mwanza Dk. Valentino Bangi wakati akisoma taarifa ya Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mwanza - Sekou Toure kwa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete aliyefika Hospitalini hapo 

Dk. Bangi alisema kuwa tatizo la vifo vya kina mama wajawazito na watoto limepungua kwa kiasi kikubwa katika Hospitali hiyo ukilinganisha na miaka ya nyuma kwani mwaka 2012 vifo vilivyotokana na tatizo la uzazi vilikuwa 10 ukilinganisha na mwaka 2011 ambapo kulikuwa na vifo 15.

“Kiwango cha utoaji wa chanjo kwa watoto kimeongezeka katika mkoa wetu na kufikia asilimia 95, jumla ya watoto 91194 ambao ni sawa na asilimia 85 waliolazwa walipata chanjo ya pepopunda na vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja ni vimepungua na kufikia 11 kati ya vizazi hai 1000”, alisema Dk. Bangi.

Aliendelea kusema kuwa wamefanikiwa kukarabati jengo la upasuaji, wodi ya watoto, wagonjwa mahututi wodi ya kujifungua kina mama, kuajiri watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo madaktari bingwa watano, ujenzi wa vyumba vya kuhifadhia chanjo, jengo la wagonjwa wa afya ya akili, na maabara ya kisasa kupitia msaada wa watu wa Marekani.

Dk. Bangi alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni upungufu wa dawa, vifaa tiba na watumishi wenye ujuzi, bajeti finyu katika uendeshaji wa huduma za afya, uchakavu wa majengo, kukosa mfumo imara wa rufaa kuanzia zahanati hadi hospitali ya rufaa, ukosefu wa nyumba za watumishi, kushindwa kukamilisha jengo la upasuajai la akina mama wajawazito na kuongezeka kwa makundi mbalimbali ya misamaha katika kutoa huduma za afya.


No comments:

Post a Comment