MAHAKAMA Kuu Dar es Salaam imepanga kusikiliza maombi ya dhamana ya Mwigizaji nyota wa filamu nchini, Elizabeth Michael, maarufu kwa jina la Lulu, Ijumaa ya wiki hii.
Lulu anashtakiwa kwa kosa la kumuua aliyekuwa msanii mwenzake wa fani hiyo, Steven Kanumba, bila kukusudia.
Uchunguzi uliofanywa na tovuti ya Habarimpya.com na kudhibitishwa na vyanzo vya ndani kutoka Mahakamani hapo zimedai kwamba msanii huyo anaweza kupata dhamana hiyo na kurudi uraiani.
Awali Lulu alikuwa akikabiliwa na kosa la kuua kwa kukusudia, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, lakini baada ya upelelezi kukamilika alibadilishiwa mashtaka na kuwa ya kuua bila kukusudia, kisha kesi hiyo ikahamishiwa Mahakakama Kuu, ambako ndiko
itakakosikilizwa.
Kwa sasa Lulu yuko mahabusu katika Gereza la Segerea, lakini amewasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu ,kupitia kwa jopo la mawakili wake, Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Masawe, akiomba aachiwe huru kwa dhamana wakati akisubiri uamuzi wa kesi yake ya msingi.
Habari zilizopatikana kutoka mahakamani hapo zinasema kuwa tayari maombi hayo ya dhamana yamepangwa
kusikilizwa, Januari 25 , mwaka huu, mbele ya Jaji Zainabu Muruke, wa Mahakama Kuu.
Maombi hayo yamewasilishwa kwa hati ya dharura ili yaweze kusikilizwa mapema kwa sababu kuwa kosa linalomkabili mshtakiwa huyo linadhaminika na pia kwamba mshtakiwa amekaa rumande kwa muda wa miezi saba.
Akizungumza na Habarimpya.com wakili wake, Kibatala amedai katika kiapo chake alichokiwasilisha sambamba na madai hayo kuwa anaiomba mahakama impe dhamana kwa masharti yoyote kwa kuwa yeye kama wakili wake yuko tayari , kutimiza wajibu wake.
"Wajibu wangu ni kuhakikisha kuwa mshtakiwa anatimiza masharti yote ya dhamana na kufika makamani kadri na wakati atakapohitajik"alisema Kibatala. Lulu anadaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia, April 7, 2012, nyumbani kwake (Kanumba), Sinza Vatican jijini Dar es Salaam.
CHANZO: Habarimpya.com
No comments:
Post a Comment