Monday, March 18, 2013

POLISI WAPEKUA OFISI ZA CHADEMA, LWAKATARE AFIKISHWA MAHAKAMANI

Wakati Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo, jana mchana ofisi za makao makuu ya chama hicho zilipekuliwa na polisi na kuondoka na nyaraka mbalimbali.
Tukio hilo lilitokea jana ikiwa ni mwendelezo wa upelelezi wa tuhuma zinazomkabili Lwakatare ambazo zinazomhusisha na picha ya video iliyorushwa kwenye mitandao ya kijamii. Lwakatare alikamatwa Jumatano iliyopita akihusishwa na picha hiyo iliyomwonyesha Lwakatare akiwaelekeza watu ambao hawakuonekana, kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani au uhalifu.
Polisi hao wakiwa na Lwakatare na mmoja wa mawakili wake, Nyaronyo Kicheere walikwenda kwenye ofisi za Chadema saa 9.00 alasiri kwa ajili ya kufanya upekuzi.
Upekuzi huo uliendeshwa zaidi kwenye ofisi za Lwakatare kwenye Makao Makuu ya Chadema yaliyoko Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Upelelezi wa kesi hiyo unaongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Obadia Jonas ulikuwa na lengo la kupata hati zenye mwandiko wa Lwakatare ili kufananisha na nyaraka mbalimbali walizonazo polisi. Kwa nyakati tofauti, Nyaronyo Kicheere na Ofisa Habari Mwandamizi wa Chadema, Tumaini Makene walithibitisha juu ya upekuzi huo.
CHANZO: MWNZANCHI

No comments:

Post a Comment