Friday, January 25, 2013

MWENDELEZO WA TAARIFA:WANANCHI WA KIBITI WACHOMA NYUMBA ZA ASKARI POLISI


VURUGU kubwa zilizowalazimisha Polisi kutumia helikopta kuzituliza, zilitokea jana baada ya baadhi ya wakazi wa Kata ya Kibiti kuvamia kituo kidogo cha jeshi hilo wakitaka kukichoma moto katika kile kilichoelezwa kuwa ni kutaka kulipiza kisasi cha mwenzao kukamatwa na polisi na kisha kupigwa hadi kufariki dunia juzi.

Katika vurugu hizo, wakazi hao wengi wao wakiwa ni vijana, walifunga Barabara ya Kilwa kwa zaidi ya saa tatu hivyo kukwamisha usafiri wa kwenda na kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi.

Vurugu hizo hazikuishia hapo kwani vijana hao walivamia nyumba za askari wa kituo hicho na kisha kutoa vyombo na kuviharibu. Katika tukio hilo, nyumba moja ilichomwa moto.

Hali ilivyokuwa
Kamanda wa Operesheni Maalumu ya Jeshi la Polisi nchini, Saimon Sirro alisema katika tukio hilo, nyumba hiyo ya jeshi imeteketezwa kabisa kwa moto na vyumba vinne vya nyumba nyingine walizopanga askari wengine jirani vimevunjwa... “Vijana hao walikuwa wakiingia na kutoa vyombo na nguo za askari waliopanga humo na kuzichoma moto.”

Kamanda Sirro alisema vurugu hizo zilitokea baada ya kupatikana kwa taarifa za kifo cha Hamis Athumani (30), mkazi wa Kibiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amepelekwa kutibiwa majeraha ambayo kamanda huyo alisema marehemu alidai kuyapata baada ya kupigwa na askari waliomkamata alipojaribu kuwatoroka walipomkamata kwa tuhuma za kuhusika na dawa za kulevya.

Alisema kukamatwa kwake kulitokana na operesheni ya msako wa bangi na dawa za kulevya.
Akizungumzia tukio hilo, shuhuda mmoja wa tukio hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe alisema baada ya kipigo hicho, kijana huyo alilalamika maumivu na hivyo ndugu zake walifika kituoni hapo na kumpeleka Kituo cha Afya Mchukwi.

“Hali yake iliendelea kuwa mbaya na akapelekwa Muhimbili ambako alifariki dunia jana alfajiri,” alisema shuhuda huyo na kuengeza: “Taarifa hizo zilipofika kijijini, baadhi ya vijana walikusanyika na kuanza kuhamasishana na kuanza kuziba barabara kwa matairi na kuvamia nyumba za askari na kuchoma moto.”

Baada ya ghasia hizo kupamba moto, jeshi liliamua kutumia helikopta ambayo ilitua Kibiti saa 5.50 asubuhi ikiwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wakiongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Mathei.
Kamanda Sirro alisema watu 18 wamekamatwa kwa kuhusika na vurugu hizo.

Chanzo cha vurugu
Inadaiwa kuwa Jumanne saa tatu usiku, askari wa Kituo cha Polisi Kibiti walivamia kambi ya vijana wanaodaiwa kujishughulisha na biashara ya dawa za kulevya inayojulikana kwa jina la Kosovo iliyopo Mbebetini karibu kabisa na Sekondari ya Kibiti.

Askari hao ambao baadhi ya wakazi wa Kibiti wamewaeleza kuwa ni mashujaa kwa hatua yao ya kuthubutu kuvamia kambi hiyo ambayo inadaiwa kushindikana kwa muda mrefu kushughulikiwa na askari wa Kituo cha Polisi Kibiti, walikumbana na upinzani mkali wa vijana wapatao 30 wakipinga kukamatwa kwa kiongozi wao.

Inadaiwa kuwa baada ya kumkamata, walimshambulia kwa virungu lakini kutokana na upinzani mkali waliopata kutoka katika kundi hilo, walishindwa kuondoka naye lakini walimwacha akiwa mahututi.

Habari hizo zilieleza kuwa vijana hao walimchukua kiongozi wao na kumpeleka Mchukwi kwa matibabu kabla ya kumsafirisha kwenda Muhimbili ambako alifariki dunia.

Baada ya kupatikana kwa taarifa za msiba huo, baadhi ya wananchi wa Kibiti waliandamana saa 1.22 asubuhi hadi kituo cha Polisi ambako waliharibu pikipiki tatu za polisi. Walitawanywa baadaye kwa baruti na silaha za moto.
Baadaye, polisi kutoka Ikwiriri walifika na kudhibiti kundi kubwa la watu hao wapatao 120 kwa mabomu ya machozi.

Askari afariki
Askari wa Kikosi cha Kutuliza ghasia (FFU) H21 PC Domick, amefariki dunia na wenzake wanne kujeruhiwa vibaya, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Kibaha Pwani kuelekea Rufiji kutuliza vurugu hizo kupinduka katika eneo la Mkuranga.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment