Wakuu wa majeshi wa nchi wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu ya
Afrika na Jumuiya ya Ustawi ya Kusini mwa Afrika SADC wamekutana mjini
Kampala Uganda na kuweka mikakati ya kijeshi yenye shabaha ya
kuwatokomeza wanamgambo waasi walioko katika eneo lililogubikwa na
machafuko la mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Maafisa hao
wa kijeshi wamesisitiza juu ya kufanya juhudi za kuleta amani na
uthabiti katika eneo hilo baada ya kuonekana dalili za kushindwa juhudi
za kimataifa za kuutatua mgogoro huo. Crispus Walter Kiyonga Waziri wa
Ulinzi wa Uganda amesema kwenye kikao hicho kwamba kuna ulazima wa
kukurubishwa mitazamo kwa lengo la kutatua migogoro iliyoko katika eneo
hilo. Wakuu wa nchi za eneo la Maziwa Makuu ya Afrika wanavituhumu
vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani nchini Kongo kwa kushindwa
kuchukua hatua za kimsingi za kuzuia wimbi kubwa la mamia ya maelfu ya
wakimbizi wa Kongo linaloelekea katika nchi za Uganda na Rwanda.
No comments:
Post a Comment