Saturday, December 15, 2012

20% YA BIDHA BIDHAA ZINAZOINGIA NCHINI NI FEKI


ASILIMIA 20 ya bidhaa zote zinazoingizwa nchini ni bandia, hivyo kuhatarisha maisha ya wananchi, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda amesema.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Dk Kigoda alisema kama hali hiyo itaachwa iendelee itasababisha madhara makubwa kwa wananchi na taifa kwa jumla.
Alisema kuenea kwa soko la bidhaa bandia nchini kunatokana na bei za bidhaa hizo kuwa ndogo, hivyo kuwavutia wateja wengi.
“Watanzania wenye kipato cha chini ndiyo wapenzi zaidi wa bidhaa hizi lakini wanatakiwa kutambua kuwa madhara yake ni makubwa mno,” alisema Dk Kigoda na kueleza kuwa Serikali imetangaza vita na wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa hizo.
Dk Kigoda aliwataka wafanyabiashara wanaouza bidhaa hizo kuziondoa sokoni haraka kabla Serikali haijaanza kuziondoa kwa nguvu. Waziri Kigoda alisema uchunguzi umebaini kuwa, kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo mkoani Pwani, kuna bandari bubu 32, ambazo hutumika kupakua bidhaa hizo bandia.
Alizitaja bidhaa hizo kuwa ni matairi ya magari na pikipiki, mafuta ya kupaka, maziwa ya watoto, nyaya za umeme, simu za mkononi na vyakula mbalimbali.
Alisema katika kukabiliana na hali hiyo, wizara yake inashirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kuchunguza bidhaa zinazoingia nchini kabla hazijasambazwa katika soko.
Alipoulizwa ni lini operesheni ya kuwakamata wanaouza bidhaa hizo itaanza, Dk Kigoda alimtupia swali hilo Katibu Mkuu wa Wizara yake, Joyce Mapunjo ambaye alisema huenda ikaanza leo, huku akisema wizara inachokifanya kwanza ni kutoa tahadhari. Dk Kigoda akaongeza... “Tukianza (operesheni maalumu) hatutakuwa na mjadala.”
“Zipo nyaya bandia za umeme ambazo kwa kiasi fulani zinaweza kuwa chanzo cha kuongezeka kwa matukio ya nyumba kuteketea kwa moto nchini, pia yapo matairi ya magari na pikipiki ambayo nayo kwa kiasi fulani yanachangia kuongezeka kwa ajali.”
Akitolea mfano Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Kigoda alisema kuanzia Januari mpaka Novemba mwaka huu, kulikuwa na ajali za pikipiki 1997, zilizosababisha vifo vya watu 140.
“Tumejipanga kuhakikisha jambo hili tunalimaliza kabisa, kwanza tumegundua bandari bubu 32 ambazo pamoja na mambo mengine, zinaifanya Serikali kukosa mapato na kuhatarisha usalama wa wananchi” alisema Dk Kigoda.
Alisema kuwa tayari wameshazieleza taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya kutumia bidhaa bandia yakiwamo ya hasara kutokana na kuharibika katika kipindi kifupi.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment