Wednesday, March 26, 2014

CCM wanasikilizwa, CHADEMA wanaheshimika


Katika pitapita yangu nikakutana na makala hii iliyochapishwa katika gazeti lililotupwa korokoroni la MWANAHALISI.
Nilipo isoma makala hii nikajiuliza kwenye Bunge hili Maalumu  la Katiba lenye viroja, mazingaombwe na matukio ya aibu kwa baadhi ya waheshimiwa ni nani anaesikilizwa na nani anaeheshimiwa?
Viroja vinavyoendelea katika Bunge hilo imepelekea baadhi ya wananchi kujenga shaka juu ya hatma ya upatikanaji wa katiba itakayokuwa kwa maslahi na ustawi wa wananchi na kwa Tanzania yetu tuitakayo.
Embu jikumbushe makala hii hapa chini>>>>
MWENENDO WABUNGE WETU
MKUTANO wa Bunge la bajeti unaendelea mjini Dodoma, pamoja na kwamba wananchi wengi wamekatishwa tamaa na mwenendo wa serikali, lakini bado wanaendelea kufuatilia mjadala wake.
Na kwa kadri siku zinavyosonga mbele, ndivyo watu wengi wanaelekea kujenga msimamo juu ya mwenendo wa bunge hili.

Aidha, pamoja na wingi wa vyombo vya habari; na hasa televisheni vinavyolazimika kuegemea upande mmoja wa chama tawala, bado kuna kundi kubwa la wananchi wanaofuatilia kwa umakini mijadala hii bila kuyumbishwa na habari za upendeleo za baadhi ya vyombo hivyo.
Katika kufuatilia mijadala ya wabunge wetu, mambo mawili yameendelea kujitokeza waziwazi na kuwaudhi baadhi ya wananchi.
Mambo hayo, ni upendeleo wa wazi wazi wa Spika wa Bunge, Anne Makinda na wenyeviti wa bunge kwa serikali na chama tawala.
Upendeleo huu unakwenda sambamba na ukandamizaji wa hoja za wabunge wa upinzani.
Jambo la pili, ni tafsiri potofu za kanuni za Bunge zinazotolewa na Spika Makinda, pale miongozo inapotolewa. Tafsiri hizi potofu huambatana na jazba na mihemuko ya kiitikadi kutoka kwa viongozi hawa adhimu katika muhimili huue.
Mpaka sasa, Spika na Naibu wake, Job Ndugai wanaongoza kwa maamuzi yaliyojaa jazba; wakati ambapo Ndugai anaongoza kwa matamshi yaliyojaa kashfa na kejeli zinazodhalilisha mbele ya Bunge.
Matokeo ya kasoro hizo mbili hapo juu, tayari imejengeka taswira katika jamii na hasa miongoni mwa wale wanaofuatilia mijadala bungeni, kuwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wana haki ya kusikilizwa wakati wabunge wa CHADEMA na baadhi ya wapinzani, wana haki ya kuheshimika kwa misimamo yao.
Mtizamo huu unazidi kuenea kwa kasi hata miongoni mwa wanachama wa CCM wenyewe. Hii ni kwa sababu, wengi wa wanachama wa chama hiki hata wale wa msimamo mkali na uzalendo kwa chama, wamefikia hatua ya kusema kuwa watabakia kuwa wanachama wa CCM hata kama chama kinaboronga bungeni.
Ukiwauliza wanachama hao kwa vipi chama kinaboronga, wanaorodhesha mambo mengi yakiwamo, kutosimamia maslahi ya taifa, kutoa ahadi zisizotekelezwa, kutosema kweli, kutosimamia haki na ububu kuhusu vita dhidi ya ufisadi.
Kimantiki, wanachama hawa wanasema, katika hoja nyingi zinazoibuliwa bungeni, wabunge wa CCM wanasimamia chama zaidi kuliko maslahi mapana ya taifa. Hata pale misimamo ya chama inapokinzana na maslahi ya taifa, wao husimamia maslahi ya chama au hukaa kimya.
Mifano hai ambayo wamenieleza, ni pale mbunge anaposimama kuchangia na kudai haungi mkono hoja mpaka mambo fulani yabadilishwe. Kiukweli mambo hayo huwa hayabadilishwi na mbunge huyo huishia kuunga mkono hoja na kupitisha bajeti hiyo.
Baadhi ya wabunge wa CCM huchambua bajeti na kubainisha madhaifu mengi bila hata kuonyesha uzuri hata mmoja wa bajeti hiyo, kisha humaliza kwa kuunga mkono hoja.
Tabia hii ndiyo imezalisha mtizamo wa kwamba wabunge wa CCM wana haki ya kusikilizwa lakini hawana haki ya kuheshimiwa kwa woga wao huo.
Upande wa pili unaihusu kambi rasmi ya upinzani bungeni inayoongozwa na CHADEMA ikiungwa mkono kwa karibu sana na wabunge wote wa NCCR-Mageuzi na wachache sana kutoka Chama cha Wananchi (CUF).
Wabunge hawa kutoka CHADEMA, wanashiriki bunge hili la bajeti kwa taabu sana. Wanaposimama bungeni kuchangia, huzomewa, huchekwa, hukejeliwa, hutukanwa kuwa vituko, husimamishwa kuchangia ili kusikiliza miongozo na taarifa zisizo za lazima.
Siku za karibuni hata hotuba zao zimezuiwa zisisomwe mpaka zihaririwe. Mara kadhaa wametolewa nje ya eneo la bunge kwa sababu zimegusa maslahi ya walioko madarakani.
Wapo wanaosema kuwa mbunge wa upinzani katika bunge linaloongozwa na maspika wa CCM katika Bunge la Tanzania, inakubidi kujitoa mhanga na kukubali kudhalilishwa ili kusimamia unachokiamini.
Matokeo ya udhalilishaji huu usiojali mbunge anachangia nini, kumejitokeza mambo mawili ya msingi.
Kwanza, wabunge wa CCM na kiti cha spika hawasikilizi wabunge wa upinzani wanachosema. Wanahangaika wakati wote kutafuta kanuni, na miongozo ya kuingilia uchangiaji wao.
Kwa jinsi hiyo wanapoteza fursa ya kusikiliza hoja na michango ya wapinzani. Mbunge wa upinzani akimaliza kuchangia baada ya kuruka vizingiti vyote, wabunge wa CCM na kiti cha spika, huambulia kuorodhesha kasoro za michango hiyo badala ya mchango wenye maslahi.
Nyingine huwa si kasoro bali uelewa mdogo unaoambatana na ulevi wa itikadi muflisi ya chama kushika hatamu.
Pili, wasikilizaji husikiliza kwa makini michango ya wapinzani na kukerwa na jinsi wabunge wa chama kilichopo ikulu na kiti cha spika kinavyowasumbua wanapokuwa wanachangia.
Hatua hiyo huambatana na huruma kwa wapinzani na matokeo yake huzaliwa heshima kubwa kwa michango yao.
Kimsingi wabunge wa upinzani wamejijengea heshima mbele ya bunge kwa kusimamia maslahi ya taifa na kuzungumzia kero zinazowakabili wananchi wengi.
Hali hii inawafanya waonekane ni watetezi wa wanyonge na kwa hiyo hatua yoyote ya kuwanyamazisha inawafanya wanaowanyamazisha waonekane ni wasaliti wa taifa.
Huruma ya wananchi kwa wabunge wa upinzani bungeni haitokani na unyonge wala uchache wa wabunge hao; inatokana na ukandamizaji na uonevu wa kiti cha spika kwa wabunge hao na michango yao.
Watazamaji wengi hawaoni kosa la wabunge wa upinzani, bali wanaona uonevu wa kiti cha spika. Madhara yanayotokana na uonevu huu wa kiti cha spika, yanafanyika kwa kudhani wahusika wanafanya uzalendo kwa chama chao.
Ofisi ya spika yeweza kufanya uchunguzi wa kubaini madhara ya kuwatoa nje wabunge. Ofisi hiyo itashangaa kugundua kuwa kitendo hicho kinawaudhi wapigakura bila kujali mbunge anayetolewa ni wa chama gani.
Katika tasnia ya mikakati ya kisiasa, wataalam wenye ujuzi wa kushughulikia madhara yasiyokusudiwa ni wachache.
Mfano wa miaka ya karibuni ni ushindi wa Barak Obama huko Marekani. Rais Obama alianza kimchenzo kwa kutangaza kuwania kiti cha useneta wa jimbo la Illinois.
Pamoja na kwamba mtu mweusi aliwahi kuwa seneta wa jimbo hilo, haikutegemewa kuwa Obama angeshinda uchaguzi huo kwa sababu katika siasa za jimbo hilo hakuwa maarufu na hata watu wengi wa mitaa yake.
Alitengenezewa zenge kwa kuvumishiwa amerukwa na akili kiasi cha kushinda anavuta sigara kijiweni tangu asubuhi mpaka jioni.
Lakini baada ya kushinda kiti hicho na pungufu ya miaka miwili akatangaza kuwania urais. Wengi waliangua kicheko.
Ni kwa sababu, alikuwa mweusi, maskini, asiye na uzoefu kwenye seneta, asiye ana uzoefu wa kuongoza dola na nchi ilikuwa vitani. Sababu hizo zote ziliwafanya wamarekani wengi kumpuuza wakitarajia atajitoa wakati wowote.
Lakini haikuwa hivyo. Alishiriki uchaguzi huo hadi mwisho na hivyo wapinzani wake wakajikuta uso kwa uso na uchaguzi mgumu kati ya kumchagua mweusi, kijana, na mwenye agenda yenye matumaini na kumchagua mzungu, mzee, mzoefu wa siasa za Marekani lakini asiye na agenda yenye matumaini.
Ubabe wa rais Bush na chama chake wakati ule, haukutofautiana na ubabe wa kiti cha spika katika bunge letu la sasa na CCM yake. Hatuna chanjo ya kuzuia tusipatwe na madhara yaliyowapata Wamarekani.

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 25 July 2012

No comments:

Post a Comment