Tuesday, March 25, 2014

VPL Kesho Azam Na Yanga Kusaka Alama Muhimu.

Klabu za Azam na Yanga ambazo zinachuana kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, zinashuka tena viwanjani kesho (Machi 26 mwaka huu) kuwania alama tatu.

Azam yenye alama 47 itakuwa mgeni wa Mgambo Shooting katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mgambo Shooting ipo katika nafasi ya kumi na moja kwenye msimamo wa VPL ikiwa na alama 19.
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Yanga na Tanzania Prisons kuanzia saa 10.30 jioni. Yanga ipo nyuma ya Azam kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na alama 47. Hata hivyo, timu hiyo ina mchezo mmoja mkononi.


Tanzania Prisons ambayo ipo chini ya Kocha David Mwamaja hivi sasa ina alama 22 ikiwa katika nafasi ya kumi. Timu tatu za mwisho katika ligi hiyo itakayomalizika Aprili 19 mwaka huu zitashuka kurudi Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Ligi itaendelea tena Jumamosi (Machi 29 mwaka huu) kwa mechi kati ya Ashanti United na Oljoro JKT itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.


Jumapili (Machi 30 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Mbeya City na Tanzania Prisons (Uwanja wa Sokoine), Kagera Sugar na Ruvu Shooting (Uwanja wa Kaitaba), Mtibwa Sugar na Coastal Union (Uwanja wa Manungu), JKT Ruvu na Rhino Rangers (Uwanja wa Azam Complex), Azam na Simba (Uwanja wa Taifa) na Mgambo Shooting na Yanga (Uwanja wa Mkwakwani).

No comments:

Post a Comment