Tuesday, February 26, 2013

POLISI WATUMIA NGUVU KUZUIA MAITI KUSAFIRISHWA MKOANI GEITA.

Katika tukio hilo inadaiwa kuwa kiasi cha Sh360 milioni kiliporwa. Kati ya fedha hizo, Sh60 milioni zinadaiwa kwamba zilikuwa kwenye gari wakati Sh300 milioni. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paulo.
POLISI wa Mkoa wa Geita wametumia nguvu kuzuia msafara wa waombolezaji waliokuwa na mwili wa marehemu mfanyabiashara, Yemuga Fungungu (48), mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha vurugu kubwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paulo alikuwapo wakati askari wake walipoingilia msafara huo na kusababisha vurumai kubwa.


Waombolezaji hao walikuwa wakiuhamisha mwili wa marehemu Fungungu kutoka Hospitali ya Runzewa kuupeleka katika Hospitali ya Geita.

Sakata hilo la ndugu na polisi lililotokea saa nane mchana juzi Jumamosi katika Pori la Samina, Geita na polisi wakiwa kwenye magari matatu wakiwa wamesheheni silaha mbalimbali walifika na kuzuia mwili wa marehemu kusafirishwa.

Baadhi ya ndugu wa marehemu akiwamo mkewe, wanadai kwamba Fungungu alifariki dunia baada ya kupigwa risasi na polisi wanaosemekana kwamba walimvamia nyumbani kwake usiku wa kuamkia Alhamisi iliyopita kisha kupora mamilioni ya fedha. 


Wanadai kwamba alipigwa risasi tumboni na kichwani katika Kijiji cha Runzewe, Wilaya ya Bukombe mkoani hapa.

Katika tukio hilo inadaiwa kuwa kiasi cha Sh360 milioni kiliporwa. Kati ya fedha hizo, Sh60 milioni zinadaiwa kwamba zilikuwa kwenye gari wakati Sh300 milioni zilikuwa kwenye masanduku mawili yaliyokuwa ndani ya nyumba.

Pia ndugu hao walidai kwamba Sh1.2 milioni zilichukuliwa na askari wawili wa kiume baada ya kumpekua mke wa marehemu kwenye nguo za ndani.

Pia askari hao wanadaiwa kupora mali mbalimbali za marehemu zikiwamo redio mbili, video kamera moja, nguo za marehemu ikiwamo kanzu, mashine ya printer, mashine ya inventor, karatasi za picha, deki mbili za kucheza CD, pamoja na nguo za mke wa marehemu.

Mapema Kamanda Paulo alikuwa ameeleza kuwa marehemu alijiua mwenyewe baada ya kumjeruhi Polisi, Fortunatus Beatus kwa risasi lakini taarifa hizo zimepingwa vikali na ndugu na jamaa wa marehemu ambao wanadai marehemu aliuawa na polisi akiwa nyumbani kwake.

Polisi kuzuia waombolezaji.

Baada ya polisi kuyasimamisha magari manane yaliyokuwa katika msafara huo wa kupeleka mwili wa marehemu kwenda kuhifadhiwa katika chumba cha maiti Hospitali ya Geita, kulizuka mabishano makali kati ya Kamanda Paulo na ndugu wa marehemu.

Inadaiwa kwamba polisi walikuwa wakishinikiza mwili huo urejeshwe Runzewe, Bukombe kwa kuwa tayari ulikuwa umefanyiwa uchunguzi jambo ambalo liliwakera waombolezaji hao.

Kabla ya kamanda huyo kufika eneo hilo, msafara huo ulisimamishwa na Polisi wa Usalama Barabarani ambao walikuwa wamefuatana na wale wa Kutuliza Ghasia (FFU), wakiongozwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Geita, Leonard Makona.


Baada ya kuusimamisha msafara huo, Makona aliwataka ndugu wa marehemu kumsubiri Kamanda Paulo ambaye alifika baada ya takriban dakika 10.

Mwandishi wa habari hii ambaye alikuwa katika eneo la tukio, alishuhudia ndugu wa marehemu na Kamanda Paulo wakirushiana maneno.

“Mnapeleka wapi mwili wa marehemu, ina maana hamkuridhika na uchunguzi wa daktari wa Bukombe?” alihoji kwa ukali na kujibiwa pia kwa ukali na kaka wa marehemu, Mariatabu Fungungu: “Kwa nini mnatusimamisha ?. 


Tunaomba tuite waandishi wa habari hapa ili waje washuhudie tukio hili. Kwa nini msikae ofisini ?”.

CHANZO: http://www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment