Wednesday, February 13, 2013

JK AWATOSA CC WAWANIA URAIS 2015


MWENYEKITI wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ameamua kuwatosa vinara wanaotajwa kutaka kuwania urais kupitia chama hicho kutoingia kwenye Kamati Kuu (CC).
Dalili za kuwatosa vinara wanaotajwa kuwania urais 2015, ni kutokana na hatua yake ya juzi kuamua kutowapendekeza kuwa miongoni mwa majina ambayo yangepigiwa kura ili kuweza kuingia katika CC.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa ndani na nje ya CCM wanaona hatua ya Kikwete kutopendekeza majina ya wanasiasa vigogo wanaotaka urais 2015 kupitia chama hicho katika orodha ya watu 42 ili kuwania nafasi 14 za CC kama mkakati maalumu wa kuwaweka kando.

Hata hivyo, mkakati huu wa Kikwete ulikuwa hatua muhimu kwake kama kiongozi wa chama baada ya kukwama kuzuia makundi kung’ara katika chaguzi zilizopita ambapo wafuasi wa Edward Lowassa waliibuka kidedea kuanzia katika NEC, mikoani na Jumuiya za chama hicho.
Ndiyo maana baada ya kumalizika Uchaguzi wa wajumbe wa NEC, Kikwete alisita kuunda CC kwa maelezo kwamba waliochaguliwa walikuwa wageni na alikuwa hawafamu vizuri. Hatua hii ya Kikwete ilitafsiriwa kama mkakati wa kuzima nguvu ya mojawapo ya kambi.

Hata hivyo, kuna mtazamo tofauti kwamba hatua ya Kikwete kutopendekeza majina makubwa na yenye nguvu ndani ya CCM kuwania ujumbe wa Kamati Kuu inaweza ikawa ni njia ya kuwafanya wajumbe wa CC kuwa na kazi moja tu ambayo ni kuchuja majina ya wagombea badala ya wao pia kuwa washiriki.
Bebard Membe, Samuel Sitta na Edward Lowasa

Katika hali iliyozua gumzo, majina ya wanasiasa vigogo Edward Lowassa, Benard Membe na Samuel Sitta ha yakuwamo katika orodha ya Rais Kikwete aliyowasilisha mbele ya NEC ili kupata wajumbe wa CC, ambacho ni chombo muhimu cha uamuzi ndani ya chama hicho.

Lowassa, Membe na Sitta ndiyo wanaelezewa kuwa na makundi makubwa yana yowaunga mkono kiasi cha kutishia uhai wa chama hicho katika chaguzi zijazo.
Makundi ya watu hao yamekuwa hasimu kiasi cha wakati fulani, Kikwete kulazimika kuunda kamati ya watu watatu chini ya Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Makamu Mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Pius Msekwa na Abdulrahman Kinana, ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho kwa sasa ili kusuluhisha mgogoro huo.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment