Monday, February 4, 2013

MAANDAMANO KUSHINIKIZA DHAMANA YA SHEIKH PONDA YAANDALIWA


Sheikh Ponda Issa Ponda
Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania zimetangaza kuwa zitaandamana Februari 15, mwaka huu endapo Katibu wa Jumuiya hiyo, Shekh Ponda Isa Ponda, pamoja na wenzake walioko gerezani hawatapewa dhamana Februari 14.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Amiri Mkuu wa Shura ya Wahadhiri Tanzania, Kondo Bungo, wakati wa kongamano la mwendelezo wa kuwainua Waislamu waweze kudai haki zao lililofanyika katiak viwanja vya Shule ya Sekondari ya Nuruyakin, Temeke, jijini Dar es Salaam.
 
“Kupewa dhamana ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania, haiwezekani hadi leo (jana) wenzetu wanasota jela kwa kosa la kutetea haki zao na wakati wapo watu waliotuhumiwa kuua wamepewa dhamana, lakini Waislamu wananyimwa, kwa sasa hatutakubali, lazima kieleweke,” alisema Bungo.
 
Alisema kama dhamana haitapatikana siku hiyo, wataandamana hadi kwenye ofisi za Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwani aliyewanyima dhamana viongozi wao ni yeye (DPP)na siyo mahakama.
 
Sheikh Bungo alisema wapo viongozi wengi wa Kiislamu kutoka bara na visiwani waliokamatwa kwa sababu ya kutetea haki za Waislamu na badala yake kubadilishiwa makosa wanapofikishwa mahakamani ili ionekane kuwa wana makosa.

No comments:

Post a Comment