Saturday, October 12, 2013

TEA YATOA SHILINGI MILIONI 880 KWA WANAFUNZI WA KIKE VYUONI

MAMLAKA ya Elimu Tazanzania (TEA) imefadhili Sh milioni 879 katika vyuo tisa vya ufundi kuongeza uwezo wa wanafunzi wa kike katika masomo ya sayansi nchini ambao hawakupata fursa ya kujiunga na kidato cha tano. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Meneja Habari Elimu na Mawasiliano, Sylvia Lupembe alisema wanafunzi 1861 waliosoma masomo ya sayansi kupitia mpango huo wemefanikiwa kujiunga na elimu ya juu.

Lupembe alisema katika mpango huo wanashirikiana na Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) na zimetolewa Sh milioni 200 katika Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa awamu ya kwanza ya mpango huo.

“Tumefanya makubaliano na TCC kwa miaka mitatu na kwa awamu ya kwanza wametufadhili Sh milioni 200 na awamu ya pili wamekubali kuwafadhili wanafunzi watakaofanya vizuri zaidi na kujiunga na masomo ya shahada.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Meneja Mawasiliano na Misaada kwa Jamii wa TCC, Martha Saiveiye alisema wamevutiwa kufadhili mpango huo kutokana na upungufu wa wanasayansi wa kike nchini.

Saiveiye alisema anaamini wasichana wanaweza kufanya vizuri katika masomo ya sayansi kama watawezeshwa.

“TCC tupo kwa ajili ya kusaidia jamii hivyo tuliona ni vema tuwasaidie wasichana hao waweze kutimiza malengo yao ya kuwa wanasayansi,” alisema.

No comments:

Post a Comment