Amefafanua kuwa CCM inaua ubunifu wa vijana, kwamba asilimia 90 ya wanafunzi wanafeli shuleni huku viongozi wa chama hicho wakiwahadaa wananchi kwamba wanaleta maendeleo.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana alipozuru Shirika la Anga la Marekani (NASA) huko Huntsville nchini Marekani, ambako anaendelea na ziara yake ya kujifunza katika majimbo mbalimbali.
Akiongozana na mkewe, Josephine Mshumbusi, katibu mkuu huyo alilakiwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Charles Frank Bolden Jr. pamoja na watendaji wengine na kupata fursa ya kutembezwa sehemu kadhaa.
Dk. Slaa alifika hapo kujifunza mambo mbalimbali, ikiwamo namna ya kuwashirikisha na kuwapa vijana wa Kitanzania changamoto ili waweke jitihada zaidi kwenye masomo ya sayansi, waweze kuinyanyua Tanzania kutoka kwenye shimo la umaskini.
Taarifa zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, zilimnukuu Dk. Slaa akisema kuwa wanasayansi wa Kimarekani walifika mwezini baada ya kupata changamoto kutoka kwa aliyekuwa Rais wao, John F. Keneddy, aliyewaomba wanasayansi hao kufikisha mtu mwezini chini ya miaka 10.
Alisema kuwa wanasayansi hao walimjibu na kufika mwezini chini ya miaka minane. Hali aliyodai ilitokana na Serikali ya Marekani kuipa kipaumbele elimu.
Dk. Slaa alisema kuwa baada ya uhuru, hayati Mwalimu Nyerere aliipa kipaumbele elimu kwa ujumla. Akitolea mfano kwamba aliwachukua vijana watano wanajeshi na kuwapeleka nchini Ireland kusomea mambo ya uhandisi.
“Waliporudi walipelekwa Kibaha ambako walibuni na kutengeneza gari la kwanza lililoitwa Nyumbu, ambalo ni ubunifu wao.
“Baadaye Mwalimu Nyerere aliwabunia wanajeshi hao mradi wa dhahabu wa Buhemba, ambao ungewawezesha kulipia gharama za kutengeneza magari mengi,” alisema.
Katibu mkuu huyo aliongeza kuwa kwa bahati mbaya baada ya Mwalimu kustaafu, mafisadi walijipenyeza na kuuchukua mradi huo. Kwamba huo ndio ufisadi uliozaa Meremeta.
“Mradi wa Nyumbu ukafa na kilichotokea ni ufisadi wa sh bilioni 155 uliohusisha Benki ya Netherlands ya Afrika Kusini. Hadi leo hakuna maelezo licha ya fedha hizo kutumika kwenye kampeni za CCM za mwaka 1995,” alisema.
Dk. Slaa alihoji ni maendeleo gani wanazungumzia CCM wakati watoto hawajui kusoma wala kuandika, huku wanajeshi waadilifu, wabunifu, wazalendo na wanaojituma wamefikia kuishi maisha ya ajabu.
“Ubunifu wao kama mradi wa Nyumbu umeuawa na CCM, imefanya maisha yao kuwa magumu na ya kusikitisha. Wanajeshi waliostaafu wamebaki kama ombaomba.
“Wale wanaoshiriki kulinda amani nje ya nchi wanadhulumiwa hela zao pale wanaporudi Tanzania. Nchi ambayo haiwezi kuwahudumia wanajeshi wake ni nchi isiyofaa kuwa katika ramani ya dunia,” alisema.
Dk. Slaa aliwaomba wanajeshi na vijana kutokata tamaa wala kusikitika kwani CHADEMA inasikia vilio vyao, na kwamba wanatambua kuwa ugumu wao wa maisha umesababishwa na CCM.
“Wakati hao CCM wanajineemesha na hela zetu za kodi, wanajeshi na wananchi kwa ujumla wanashindwa hata kujenga nyumba ya kujisitiri punde wanapostaafu,” alisema.
Aliongeza kuwa CCM imeua ubunifu ndani ya Tanzania na kuamua kuwaweka vijana kuwa mazezeta ili waendelee kuwatawala.
“Wenzetu wanapeleka watu mwezini, lakini Watanzania hata wembe tunanunua kutoka nje kwa sababu ya CCM. Wakiendelea kuwanyima wananchi haki zao za msingi muda utafika watachoka,” alisema.
CHANZO: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment