Friday, October 11, 2013

TANGANYIKA ONE : INAWATAKIA WAISLAM WOTE MAANDALIZI MEMA YA IDD EL-HAJ; Umuhimu wa Arafah

ALLAH Subhaanahu Wata’ala ametuneemesha na kutupa uhai tukaweza kufikia siku kumi bora kabisa katika dunia ambazo Allaah Subhaanahu Wata’ala ameziapia katika Qur’aan, Suuratul Fajr. Na Subhaana anapoliapia jambo lolote basi huwa lina umuhimu mkubwa na wa kipekee.

Neema hii ya kuwa tupo hai na tuna afya njema ni jambo kubwa na muhimu sana kwa kila Muislamu kuzingatia.

Tayari tupo katika masiku kumi bora katika mwezi wa Dhul Hijjah, kitu gani tumenufaika nacho ndani ya masiku haya? Au siku hizi zinatupita tu kama siku nyengine za kawaida?

Mtume Muhammad Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam anasema katika hadithi iliyopokelewa na Muslim kwamba: Hakuna siku ambayo Allaah (Subhaanahu Wata’ala) huwaachia waja (wake) huru na moto kama siku ya Arafah

Allaah Subhaanahu Wat’ala katika riwaya nyengine anasema kuwaaambia Malaaikah kwamba washuhudie jinsi Allaah Subhaanahu Wata’ala alivyowasamehe waja wake. Mpaka Malaaikah katika kujaribu kuhakikisha waliuliza ‘ Ee Allaah fulani amegubikwa na maasi na madhambi aina kwa aina! Allaah Subhaanahu Wata’ala atawajibu, ‘Nimewasamehe wote’

Umuhimu wa siku ya Arafah unaweza kueleweka vizuri kutokana na mazungumzo aliyobahatika kukabiliana nayo Amiirul Muuminiyn ‘Umar bin Khattab, Allaah amuwie radhi, na myahudi mmoja aliekuwa akiishi Madina wakati huo.

Siku moja Myahudi alikuja kwa ‘Umar na kumwambia ‘Kuna aya katika kitabu chenu (cha Qur’aan) mnaisoma, lau kama aya hii ingeliteremshwa kwetu Mayahudi basi siku ya kuteremshwa kwake ingelikuwa siku kubwa sana kwetu ya kushereheka’ ‘Umar akamuuliza ni aya gani hiyo? Myahudi akamsomea

: ( الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمْ الْإِسْلَامَ دِينًا) [ سورة المائدة:5

Leo nimekukamilishieni dini yenu na kutimiza neema zangu kwenu na nimeridhia UIslamu kuwa ndio Dini yenu. Al Maaidah 5

‘Umar akasema, 'bado naikumbuka siku ambayo aya hii iliteremka ilikuwa ni siku ya Ijumaa na Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam akihutubia tulipokuwa Arafah'

Naam myahudi ameonesha thamani kubwa kuithamini siku bora kabisa katika siku za dunia, Je mimi Muislamu na  wewe ndugu yangu Muislamu unaesoma ujumbe huu umewahi kuipa thamani inayostahiki siku ya Arafah ?.

Ni siku ambayo Dini yetu ilikamilishwa, ni siku ambayo Allaah huwaachia huru na moto waja wake, ni siku ambayo Allah Subhaanahu Wata’ala hutulipa thawabu za miaka miwili kwa kufunga siku hii moja tu, ni siku ambayo tukiomba dua basi Allaah atatukabalia dua zetu, ni siku ambayo Shetani anaichukia anapoona Rehma za Allaah Subhaanahu Wata’ala zinavyomwagwa kwa waja  na hujawa na tahayari na ghera mpaka kufikia kujitia mchanga usoni kwa soni na tahayari kama alivyosimulia Mtume Swalla Allaahu ‘Alayhi Wasallam katika hadithi iliyopokelewa na Ahmad.

Ndugu yangu katika imani, tuwe pamoja katika kufanya mambo ya kheri katika masiku kumi ya kheri na tuhakikishe tunatia Nia ya kufunga siku ya Arafah.

Tuwakumbushe na wengine umuhimu wa kuifunga siku hii na tumuombe Subhaana atawafikishe tuifikie siku hii adhimu katika hali ya afya na siha na kutuwezesha kufunga kwa ajili ya kupata radhi zake Subhaana.
Aamiyn Aamiyn

No comments:

Post a Comment