Thursday, September 12, 2013

KIKWETE: MTAAMBUKA BAADA YA 2015

 
Rais Jakaya Kikwete amesema wale wote wanaombeza kuhusu utendaji wake, wataona aibu atakapomaliza muhula wake 2015 huku akiwananga baadhi ya wanaCCM kwa kushindwa kuyaelezea mafanikio ya Serikali chini ya chama hicho.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme katika mikoa ya Mwanza na Geita unaofadhiliwa na Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC), Rais Kikwete alisema: “Wakati wa kampeni nilibezwa sana, lakini sasa ninawaomba walionibeza kufika vijijini na kuangalia ukamilishaji wa ahadi zangu.
“Nataka waje waone, kwa sasa ninakamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote ili kufikia lengo la Watanzania asilimi 30 kufikiwa na nishati hiyo. Hadi 2015 umeme utakuwa umesambaa nchi nzima.
“Serikali yangu itavunja rekodi ya kusambaza umeme katika vijiji vingi nchini…Tumejenga mtandao wa barabara kwa sasa, hali yetu ya barabara ni bora Afrika Mashariki, tuliahidi meli Bukoba naomba niwaeleze kuwa zinakuja, tena siyo moja ni meli mbili.
Septemba 2 mwaka huu, Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ilitangaza kuanza kwa awamu ya pili ya usambazaji wa umeme vijijini, mpango ambao utagharimu Sh881 bilioni na kukamilika Juni 2015.
Katika utekelezaji wa mradi huo, huduma za jamii zitakazopewa kipaumbele katika kuunganishiwa umeme ni shule, zahanati, misikiti, makanisa na visima vya maji.
Mpango huo unatarajiwa kuinufaisha mikoa 24 ya Tanzania Bara, huku wateja 250,000 wa awali wakiunganishwa pamoja na kuhusisha kazi ya usambazaji umeme kwenye makao makuu ya wilaya 13 zisizokuwa na umeme.
Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Balozi Ami Mpungwe alisema tayari mikoa 14 imepata makandarasi na ujenzi wa vituo sita vya usambazaji umeme, wakati mchakato wa kuwapata wajenzi katika mikoa 13 iliyokosa wakandarasi awali, unaendelea.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment