Thursday, September 26, 2013

AL-SHABAB WAZIDISHA HOFU KENYA


 

KUNDI la kigaidi la Al-Shabaab ambalo limejigamba kutekeleza shambulizi lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 67 na wengine 175 kujeruhiwa katika jengo la kibiashara la Westgate, limezidisha hofu kwa kudai kuwa mateka 137 wameuawa.

Hata hivyo, idadi hiyo imekuwa vigumu kuithibitisha kutokana na kutofautiana na ile iliyotangazwa na Serikali ya Kenya.
Katika ujumbe waliouweka kwenye mtandao wa kijamii wa twitter jana, kundi hilo limedai mateka 137 waliokuwa wanashikiliwa na Mujahedeen walikufa.
Al-Shabaab pia waliwashutumu wanajeshi wa Kenya kwa kutumia vifaa vya kemikali kukomesha mkwamo huo uliodumu kwa siku nne.


“Katika hatua ya woga wa dhahiri, vikosi vya Kenya kwa makusudi vilitumia vilipuzi vilivyokuwa na kemikali,” ulisema ujumbe mmoja na kuongeza kuwa, “ili kufunika uhalifu wao.”
Kwamba Serikali ya Kenya ililiporomosha jengo hilo na kuuzika ushahidi na mateka wote chini ya vifusi.
Kundi hilo lilisema kuwa lilifanya shambulizi hilo katika kulipiza kisasi dhidi ya Kenya kutokana na kujiingiza nchini Somalia kupambana na wanamgambo hao.

Wakati Wakenya wakiendelea na maombolezo ya siku tatu tangu jana, serikali za Marekani na Uingereza zimetoa msaada wa makachero kusaidiana na makachero wa Kenya katika kufanya uchunguzi juu ya suala hilo.
CHANZO: T/DAIMA

No comments:

Post a Comment