Friday, September 27, 2013

WARIOBA: "HAKIKISHENI KATIBA MPYA NI YA MAONI YA WANANCHI" ASEMA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA INAMAPUNGUFU

 
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko, Jaji Joseph Warioba amesema Watanzania hawatatendewa haki kama itapatikana Katiba Mpya ambayo haijatokana na maoni yao. “Hakikisheni Katiba Mpya inayopatikana ni ya maoni ya wananchi,” alisema jana muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana
.
Jaji Warioba alisema maoni yaliyomo katika Rasimu ya Katiba yametokana na maoni ya wananchi, hivyo lazima yalindwe ili kudumisha amani... “Kilichomo katika Rasimu ya Katiba ni maoni ya wananchi, wasije wakafanya makosa ya kutoa maoni haya. Haya yametoka kwa wananchi na wao ndiyo watakuwa na sauti ya mwisho kuhusu mchakato huu,” alisema na kuongeza: “Wahakikishe kwamba mawazo yaliyotolewa na wananchi yanaingia katika Katiba Mpya, wasithubutu kuyatoa maana wananchi wanaweza kukataa hali hiyo.”

 Wakati wananchi wa kada mbalimbali wakishinikiza Rais Jakaya Kikwete kutokusaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2013, kwa maelezo kuwa una kasoro, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba naye amesema sheria ina upungufu.


Warioba alisema jana kwamba ni jambo la kushangaza sheria hiyo kueleza kuwa tume hiyo itavunjwa baada ya kukabidhi Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu la Katiba, wakati huohuo ikieleza kuwa itahusika tena kusimamia utoaji wa elimu ya kura ya maoni.
Kauli hiyo ya Warioba imekuja wakati vyama vya NCCR Mageuzi, Chadema na CUF, vikifanya mikutano nchi nzima kuwashawishi wananchi kupinga kile wanachokiita hujuma dhidi ya upatikanaji wa Katiba Mpya.
Sheria hiyo ambayo Warioba amesema ina upungufu, muswada wa marekebisho yake ulijadiliwa na kupitishwa wa wabunge Septemba 6, mwaka huu katika Mkutano wa 12 wa Bunge Mjini Dodoma, ikiwa ni baada ya kubadilishwa kwa baadhi ya vifungu na hivi sasa Rais Kikwete anasubiriwa kuusaini ili iwe sheria kamili. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Jaji Warioba alisema: “Mwisho wa kazi ya tume ni baada ya kukabidhi rasimu, hilo ni tatizo. Maana tume itakuwa imeshavunjwa, sasa itafanyaje kazi ya kutoa elimu kwenye kura ya maoni?”
Jaji Warioba pamoja na kukiri upungufu huo, alisema kurekebisha au kutokurekebisha kasoro hizo si jukumu la tume hiyo.
“Tunawaomba watafakari, waone jinsi gani tume ambayo imekwishavunjwa itakuja kutoa elimu wakati wa kura ya maoni, sheria ina ‘contradiction’ (ina mkanganyiko),” alisema.

No comments:

Post a Comment