Watu watano wameuawa na wengine 12 kujeruhiwa katika vurugu zilizotokea kati ya vijana na askari wa usalama mjini Cairo nchini Misri.
Hayo yamethibitishwa na Wizara ya Afya ya Misri ambayo imeongeza kuwa, watu hao waliuawa na kujeruhiwa katika vurugu zilizotokea katika eneo la Shubra El-Kheima kaskazini mwa mji mkuu huo.
Ripoti hiyo imesema kuwa, ufyatulianaji risasi ni moja ya sababu za mauaji hayo. Duru za habari zinaarifu kuwa, vurugu hizo zilitokea baada ya mauaji ya kijana mmoja aliyeuawa na askari kwa bahati mbaya wakati akimkimbizwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na ulanguzi wa madawa ya kulevya. Kufuatia hali hiyo kulizuka vurugu zilizodumu kwa masaa kadhaa kati ya familia za marehemu na askari na kuwalazimu askari hao kutumia mtutu wa bunduki kuwatawanya watu hao waliokuwa wanakusudia kuvamia kituo cha polisi katika eneo la tukio. Tukio hilo la mauaji linajiri siku chache tu tangu kufanyika kwa sherehe za mapinduzi yaliyopelekea kung'olewa madarakani utawala wa dikteta Hosni Mubarak anayehudumia kifungo cha maisha katika jela za nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment