Monday, January 21, 2013

Mlemavu anayeteseka baada ya kubakwa

“Bibi mimi huingiliwa na mwanamume  aitwaye Mashoto, ila kaniambia nisimtaje, ikitokea nimemtaja basi atanichinja ndiyo maana nilinyamaza, nikiogopa kuchinjwa,” anaeleza Mwajabu akimnukuu Aisha alipotaka kujua aliyempa ujauzito.


SIKU hizi kuna watu wanasema; “Ni heri ukutane na mnyama mkali kama, simba au chui unaweza kusalimika, kuliko kukutana na binadamu, kwani anaweza kukudhuru.”
Maneno haya yanatokana na unyama wanaofanyiana  wenyewe kwa wenyewe. Kila siku tunasikia unyama unaofanywa na binadamu, leo utasikia baba wa miaka 45 amemnajisi mtoto wa miezi minne, mke amemkata na shoka hawara wa mume wake, majambazi wameua familia nzima na mambo kama hayo.
Hayo yanadhihirishwa na mkasa  wa Aisha (siyo jina lake halisi), aliye na  ulemavu,  ambaye hajiwezi kwa lolote bila msaada wa mtu.
Hata hivyo, pamoja na hali aliyonayo, bila chembe ya huruma, Aisha amekuwa mwathirika wa unyama wa binadamu, baada ya kubakwa.
Binti huyo anaishi katika Kijiji cha Ntisi, Kata ya Bicha, umbali wa kilometa tano kutoka Kondoa Mjini, eneo ambalo hakuna usafiri mwingine unaoweza kukufikisha zaidi ya bodaboda.
Katika kijiji hicho hakuna asiyemfahamu binti huyo kutokana na hali yake na historia ya maisha yake, ambayo inasikitisha kila aliye karibu naye.
Kwa takriban miaka 21, binti huyo ameishi na bibi yake aitwaye Mwajabu Haji, lakini sasa familia hiyo imeongezeka, baada ya Aisha kujifungua mtoto, ambaye ni zao la kubakwa. Mtoto huyo sasa ana umri wa miaka sita.
Ukifika nyumbani kwao utamkuta Aisha amekaa katika kiti chake maalumu cha mbao, alichotengenezewa na bibi yake.
Hana kiungo chochote mwilini mwake kinachoweza kufanya kazi zaidi ya mdomo wake.
Hata hivyo, inzi humwingia mdomoni na kutoka, wakirukaruka katika mwili wake wapendavyo, kwani binti huyo hawezi kuwafukuza kwa kuwa mikono yake haifanyi kazi.
Umbile lake lilivyo
Zaidi ya kuzungumza, Aisha hawezi kufanya shughuli yoyote kutokana na kuwa, mikono na miguu vimejipindapinda. Tumbo lake limesogea upande wa kushoto na kichwa  kulia.
Mara nyingi anapoongea mikono hupata nguvu ya ajabu ambapo huanza kurukaruka huku na kule kwa kuwa hawezi kuizuia, hujigonga na kujiumiza katika sehemu mbalimbali.
Mikono hiyo haina nguvu ya kuweza kubeba kitu chochote  au kufukuza wadudu wanaotambaa katika mwili wake hasa inzi kutokana na vidonda vilivyojaa.
Historia ya maisha yake
Aisha  alizaliwa mwaka 1990 Musoma, mkoani Mara akiwa na ulemavu. Alipofikisha umri wa mwaka mmoja, alipelekwa kwa bibi yake mzaa mama, baada ya baba yake kukataa kuendelea kumlea. “Kwa kweli ninamshukuru Mungu na bibi yangu kwa kiasi kikubwa,  kwa kuwa katika historia yangu, nimekutana na changamoto nyingi, lakini hakunitupa au kuninyanyapaa,” anasema na kuongeza:
“Ninamhurumia bibi kwa kuwa pamoja uzee, lakini hana budi kubeba, jukumu la kututafutia riziki ya kila siku kwa ajili yangu na mtoto wangu.
Natamani ningekuwa na uwezo hata wa kumsaidia kuosha vyombo,” anasema Aisha.
Anasimulia kuwa, kwa mujibu wa bibi yake, mama yake alilazimika kumrudisha kijijini hapo, baada ya baba yake kutaka wamchinje au wamtupe.
Aisha anaeleza kwamba, kwa kuwa mama yake alikuwa akiipenda ndoa yake, hakuwa tayari kumtupa au kumuua badala yake alimpeleka kwa bibi yake, ili kuokoa uhai wake.
“Mama yangu mzazi aliwahi kupigwa na baba,  huku akitishiwa kuachwa endapo atanilea, ndugu zake baba walimshauri anitupe,” anasema Aisha.
Anaongeza kuwa, hajawahi kukutana na baba yake mzazi, lakini anadai kuwa anamfahamu kwa jina la David Chacha akieleza kuwa anafanya kazi ya upishi jeshini huko Monduli.
Mama yake mzazi ambaye pamoja na kumrudisha kwa bibi yake, alikuwa akifika kijijini hapo mara kwa mara kumjulia hali, hata hivyo alifariki mwaka 2011.
Alivyobakwa mpaka kupata ujauzito
Kutokana na umbile lake lilivyo na pilikapilika za bibi wa Aisha katika kutafuta riziki, ilimchukua miezi saba bibi huyo kugundua kuwa mjukuu wake ana ujauzito.
Bibi huyo anasema kuwa aligundua kuwa mjukuu wake ana ujauzito, wakati tayari imeshafikisha miezi saba.

CHANZO: MWANANCHI

1 comment:

  1. Huu ni unyama usiosemeka na wa kikatili. Mimi nafikiria kuwa matukio kama haya sio ya kuyafumbia macho. Lazima tuyapinge kwa nguvu zote na njia yeyote ile. Pia kama kuna njia ya kumsaidia muathirika ingekuwa vizuri sana.

    ReplyDelete