Utangulizi
Ndugu wananchi;
Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa
rehma, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha
kuwasiliana kupitia utaratibu wetu mzuri tuliojiwekea wa kufanya hivyo
kila mwisho wa mwezi. Leo nimepanga
kuzungumza nanyi mambo matatu; yaani Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Uhusiano wa Waislamu na Wakristo na Matokeo ya
Mtihani wa Kidato cha Nne.
Mpango wa
Amani, Usalama na Ushirikiano wa
Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo
Ndugu Wananchi;
Tarehe 8 Februari, 2013 kule Addis
Ababa, Ethiopia niliungana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban
Ki-Moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mhe. Nkosozana Dlamini
Zuma na viongozi wa nchi 12 za Afrika Mashariki, Kati na Kusini kutia saini
Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na
jirani zake. Pamoja na Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo zilikuwepo nchi za Burundi, Rwanda, Uganda, Sudani Kusini,
Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Angola, Zambia na Tanzania ambazo
ni jirani ya Kongo. Nchi za Ethiopia,
Msumbiji na Afrika ya Kusini pamoja na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika
zilitia saini kama wadhamini. Ethiopia
kwa nafasi yake ya kuwa Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika na Msumbiji kwa
kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Nchi wanachama wa Mkutano wa Ukanda wa Maziwa
Makuu ziliwakilishwa na Uganda ambayo ni Mwenyekiti wake wa sasa. Afrika ya Kusini ilishirikishwa kwa kuwa
taifa kubwa na linalotegemewa katika
ukanda wetu.
Mpango huu ni jitihada nyingine ya
kusaidia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ipate amani ya kudumu. Kama tujuavyo, tangu mwaka 1997 wakati wa
vita vilivyosababisha kuondolewa kwa Rais Mobutu Seseseko mpaka sasa nchi hiyo
rafiki na jirani haijapata amani na utulivu wa kudumu. Kumekuwepo jitihada na mipango kadhaa ya
kuleta amani ambayo hata hivyo baada ya muda fulani machafuko hutokea tena na
mipango hiyo kuvurugika. Inakadiriwa
kuwa takriban watu milioni 5.4
wamepoteza maisha na watu wengi kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi yao. Pia kumekuwepo na vitendo vya ukatili dhidi
ya wanawake na watoto pamoja na mali nyingi kuharibiwa au kuporwa.
Ndugu Wananchi;
Machafuko yaliyoanzishwa na waasi wa
Kundi la M23 mapema mwaka wa jana ndiyo sababu ya kuwepo kwa Mpango huu wa sasa
tuliotia saini kule Addis Ababa, Ethiopia tarehe 8 Februari, 2013. Katika Mpango huo Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Kongo na jirani zake, Tanzania ikiwemo, tumekubaliana kutokufanyiana vitendo
vinavyohatarisha amani na usalama wa nchi zetu.
Tumeazimia tusifanye hivyo ama moja kwa moja kama nchi au kwa kutumia watu
wengine. Aidha, tumekubaliana tusiruhusu
watu au vikundi vya watu kutumia nchi zetu kuhatarisha usalama wa nchi
nyingine. Kimsingi tumekubaliana kuwa
majirani wema. Katika Mkataba huo,
majukumu ya kila nchi yameainishwa vizuri pamoja na yale ya Umoja wa Mataifa,
Umoja wa Afrika na Mashirika ya Kikanda hususan SADC na ICGLR.
Ndugu Wananchi;
Niliamua kukubali kushiriki na kutia
saini Mpango ule kwa kutambua ukweli kwamba sisi majirani wa nchi ya Kongo
tunao wajibu wa kusaidia kwa kile tunachoweza.
Wananchi wa Kongo wameteseka kwa muda mrefu mno hivyo kama Mpango huu
utawasaidia kupata amani na usalama hatuna budi kuunga mkono. Ni kwa misingi hiyo hiyo, tulikubali
kuchangia kikosi kimoja katika Jeshi la Kimataifa la kulinda amani huko
Mashariki ya Kongo kama ilivyoamuliwa na Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu mwezi
Julai, 2012. Uamuzi huo umeungwa mkono
na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa
Afrika. Umoja wa Mataifa umeamua Jeshi
hilo liwe sehemu ya Jeshi la Umoja wa Mataifa la Kulinda Amani nchini Kongo
(MONUSCO) jambo ambalo sote tumeliafiki.
Tumepeleka walinzi wa amani Darfur, Sudan na Lebanon, kwa nini
tusipeleke Kingo. Miaka ya nyuma
tulishapeleka walinzi wa amani Liberia, Siera Leon na Eritrea.
Ni matumaini yetu kuwa Mpango huu mpya
utatekelezwa kwa ukamilifu na kuzaa matunda yaliyokusudiwa. Kama nchi jirani, Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Kongo yenye amani, usalama na utulivu ni jambo lenye maslahi makubwa
kwetu. Ina maana ya kutokuwa na
wakimbizi kutoka nchi hiyo, uharamia katika Ziwa Tanganyika kutokuwepo na
ustawi wa shughuli za kiuchumi na kibiashara kwa upande wetu na wao. Ni chachu muhimu ya maendeleo ya Mikoa ya
pembeni mwa Ziwa Tanganyika na Tanzania kwa jumla.
Uhusiano wa Waislamu na Wakristo
Ndugu wananchi;
Jambo la pili ninalopanga
kulizungumzia siku ya leo ni uhusiano wa Wakristo na Waislamu hapa nchini. Kwa miezi kadhaa sasa tangu mwaka wa jana
kumekuwepo na matukio kadhaa yanayosababisha mifarakano na kupandikiza chuki
baina ya waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu. Matukio ya kauli na vitendo vya kudharau dini
za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu vya dini hizo, kuchoma moto nyumba za
ibada na mzozo kuhusu nani achinje. Kumekuwepo na matumizi mabaya ya radio na simu za
mkononi na mifumo mingine ya mawasiliano
iliyoeneza maneno na ujumbe wa chuki na vitisho kwa waumini na viongozi wa dini
zetu hizi kubwa hapa nchini. Kauli na
matendo hayo, katika baadhi ya maeneo yamekuwa chanzo cha uhasama na magomvi
baina ya waumini na hatimaye kusababisha vifo kama ilivyotokea Buseresere
Mkoani Geita na Beit-el-Ras, Zanzibar.
Ndugu zangu;
Watanzania
hatujawahi kuwa hivi, kumetokea nini? Miaka yote Watanzania ni watu tunaotambua
na kuheshimu tofauti za dini zetu mbalimbali tunazoabudu. Watanzania ni waelewa na kwa ajili hiyo
tumekuwa tunavumiliana kwa tofauti zetu na ndiyo maana tumekuwa tunaishi pamoja
kidugu, kwa umoja na kushirikiana kwa mambo yote yanayotuhusu maishani
isipokuwa wakati kila mmoja anapoingia kwenye nyumba ya ibada kumuomba Mola kwa
misingi na taratibu ya dini yake.
Watanzania wa dini zote na makabila tofauti
wanaishi nyumba moja, wanasoma pamoja, wanafanya kazi pamoja kwa udugu, upendo,
umoja na ushirikiano. Kuna koo na
familia zenye watu wa dini tofauti, wengine Waislamu na wengine Wakristo. Wapo Waislamu na Wakristo wameoana, wamezaa
na wamejukuu na kila mmoja amebakia kuwa mfuasi wa dini yake. Wapo pia ambao hawakuoa lakini wamezaa watoto
na wanashirikiana kulea watoto wao. Hayo
ndiyo maisha ya Watanzania na hiyo ndiyo Tanzania yenye amani na utulivu
tuliyozaliwa, kukua na kuishi. Nawasihi
sana Watanzania wenzangu, tuienzi na kuidumisha tunu hii waliyotujengea mababu
zetu.
Ndugu Wananchi;
Kuna
wenzetu kwa sababu wanazozijua wao na kwa manufaa wanayoyajua wao wanataka
kutuvurugia nchi yetu hii nzuri.
Tusiwape nafasi wachochezi hawa kwani hawatutakii mema na wala
hawazitakii mema dini zetu na nchi yetu.
Sisi katika Serikali hatutasita kuwachukulia hatua wale wote
wanaochochea chuki za kidini, wanaodharau vitabu vitakatifu vya dini nyingine
na wanaokejeli dini nyingine.
Nimewakumbusha Polisi na mamlaka husika
kote nchini wasifanye ajizi kwenye matukio ya namna hiyo. Wawachukulie hatua stahiki wale wote
wanaohusika. Nimewataka wazingatie msemo
wa Kiswahili usemao “ajizi nyumba ya njaa”. Wachochezi
wa mifarakano na chuki za kidini
wasipodhibitiwa ipasavyo wataleta maafa kwa Watanzania wasiokuwa na hatia. Nimewakumbusha Wakuu wa Wilaya na Mikoa kama
walinzi wa amani wa maeneo yao ya uongozi, watimize ipasavyo wajibu wao. Pia nimewataka Polisi wakamilishe mapema
upelelezi wa makosa ya vurugu za kidini na wahusika wafikishwe haraka kwenye
vyombo vya sheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Ndugu Wananchi;
Naendelea
kuwasiliana na viongozi wa dini kuzungumza nao juu ya wajibu wao maalum wa
kuhakikisha kuwa wafuasi wao hawawi chanzo au sehemu ya tatizo na mifarakano
miongoni mwa waumini wa dini mbalimbali nchini.
Hali kadhalika naitumia nafasi hiyo kuwakumbusha umuhimu wa kuzungumza
na wenzao wa upande mwingine kutatua tofauti au matatizo yanayoathiri uhusiano
mwema baina yao.
Ndugu Wananchi;
Kuna
msemo maarufu usemao “mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni
mwananchi”. Naomba tuwe wajenga
nchi na kamwe tusikubali kuwa wabomoa nchi.
Hivi tukiibomoa nchi yetu tutakwenda wapi? Tutaishi wapi? Tusikubali kugeuka wakimbizi ndani ya nchi au
nje ya nchi yetu.
Kwa mara nyingine tena, napenda kutumia
nafasi hii kuwapa mkono wa pole makanisa, familia, ndugu na jamaa wote wa
Mchungaji Kachila na Padri Mushi. Sote
tunafahamu machungu waliyonayo kwa kuondokewa na wapendwa wao. Serikali na wapenda amani wote nchini wapo
pamoja nanyi katika kipindi hiki kugumu.
Vile vile natoa rambirambi zangu nyingi kwa waumini wote wa Kanisa la
Pentekoste Assemblies of God na Kanisa Katoliki Tanzania kwa kuondolewa ghafla
na viongozi wao. Tuzidi kumwomba Mwenyezi Mungu azipumzishe kwa amani roho za
viongozi wetu. Amin.
Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne Mwaka 2012
Ndugu wananchi;
Tarehe 18 Februari, 2013 Baraza la
Mitihani la Taifa lilitangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne ya
mwaka 2012. Wanafunzi 397,132 walifanya mtihani huo na kati
ya hao, waliofaulu ni 126,851 yaani
sawa na asilimia 34.5. Wanafunzi
240,903 ambao ni sawa na asilimia 65.5 hawakufaulu mtihani
huo. Kwa ulinganifu, matokeo hayo ni
mabaya kuliko matokeo mengine ya mtihani huo ya miaka ya hivi karibuni.
Mwaka 2011, jumla ya wanafunzi 336,782 walifanya mtihani huo na
waliofaulu walikuwa asilimia 53.6 na
ambao hawakufaulu kabisa walikuwa asilimia
46.4. Mwaka 2010 jumla ya wanafunzi 352,045 walifanya Mtihani wa Taifa wa
Kidato cha Nne, asilimia 50.4 ya
wanafunzi hao walifaulu na asilimia 49.6 ya wanafunzi
hawakufaulu.
Ndugu Wananchi;
Matokeo
ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012, yameshtua na kufadhaisha watu wengi
nchini na kwa sababu stahiki kabisa.
Kwanza, kwamba kiwango cha kufaulu kimeporomoka sana, tena ghafla,
kutoka asilimia 53.6 mwaka 2011 hadi
asilimia 34.5 mwaka 2012. Hili ni anguko la asilimia 19.1 ambalo, kwa kila hali, ni kubwa sana. Pili, kwamba hata shule zinazofahamika kuwa
na historia ya kufaulisha vizuri kama vile seminari, shule za watu binafsi, za
mashirika ya dini na sekondari kongwe za Serikali ambazo hazina matatizo kama
ilivyo kwa zile sekondari za Kata, nazo safari hii hazikupata mafanikio kama
ilivyo kawaida yao. Nazo zimejikuta
zikiwa na idadi ya vijana waliopata daraja la kwanza, la pili na la tatu
ikipungua wakati waliopata daraja la nne
na waliofeli wakiongezeka.
Isitoshe na kiwango cha ufaulu wa
vijana umepungua pia. Mwaka 2010
wanafunzi 10 bora wote walikuwa
wamefaulu daraja la kwanza la alama au pointi 7. Mwaka 2011 katika wanafunzi 10 bora wanane walipata daraja la kwanza kwa alama 7 na wawili alama 8. Mwaka 2012 katika wanafunzi 10 bora, watatu walipata daraja la kwanza kwa alama 9, watatu alama 10 na
wawili alama 11.
Ndugu Wananchi;
Haya ndiyo mambo yanayozua maswali kwa
watu wengi yanayohitaji kupatiwa majawabu ya uhakika. Kulikoni mwaka 2012? Ndiyo msingi wa uamuzi wa Waziri Mkuu, Mhe.
Mizengo Pinda, kuamua kuunda Tume ya kuliangalia suala zima la mitihani ya
mwaka 2012 na matokeo yake. Hali hii
haijawahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni. Ni suala muhimu sana kwa maendeleo ya nchi
yetu, hivyo lazima ukweli wake ujulikane kwa uhakika. Hii itawezesha Serikali na wadau wengine
kuchukua hatua stahiki kurekebisha mambo mapema iwezekanavyo ili hatimaye mambo
yawe mazuri siku za usoni. Tusipofanya
hivyo mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi na lawama zinaweza kuwa kubwa zaidi kwa
Serikali.
Ndugu Wananchi;
Hivi
sasa kunatolewa mawazo lukuki kuhusu sababu za kwa nini matokeo yamekuwa
mabaya. Wapo wanaodhani kuwa lipo tatizo
katika utungaji wa mitihani, usahihishaji wake au kutoa maksi kwa watahiniwa. Wapo wanaodhani walimu hawawajibiki ipasavyo
au baadhi yao kutokumudu masomo wanayofundisha.
Wapo wanaofikiria kuwa wanafunzi hawako makini katika kufuatilia masomo
na wazazi hawajali kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni. Wapo wanaoinyooshea kidole Serikali kwa sera,
mitaala na uwekezaji usiokidhi mahitaji ya maendeleo ya elimu.
Wapo wanaofikiria kuwa Serikali kushindwa kuongeza mishahara ya walimu
kwa asilimia 100 kama walivyotaka imechangia.
Orodha ni ndefu, ali mradi kila mtu ana mawazo yake. Na sisi katika Serikali hatuwezi kuwa tunadhani
kwa sababu tunayo dhamana maalum. Lazima
tujue ukweli kwa uhakika na ndiyo maana kuna umuhimu wa Tume. Naomba kila mtu mwenye mawazo yake ayafikishe
kwenye Tume hiyo hapo itakapoundwa ili tupate jawabu muafaka la tatizo hili.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuwahakikishia kuwa sisi katika Serikali tumetoa kipaumbele cha juu sana kwa
elimu na kwamba hakuna upungufu wa utashi kwa upande wangu na wenzangu wote
Serikalini. Ndiyo maana tumeguswa sana
na matokeo haya. Bajeti ya elimu ya shilingi trilioni 3.6 ambayo ni sawa na
asilimia 24 ya bajeti yote ya
Serikali ndiyo kubwa kuliko zote. Kwa
ajili hiyo imetuwezesha kuendelea kukabili mahitaji na changamoto za upanuzi
mkubwa wa elimu ya sekondari na elimu ya juu.
Bado hatujazimaliza changamoto zote na kwamba bado tuna kazi kubwa mbele
yetu, lakini mafanikio yanaendelea kupatikana.
Tutaendelea kutoa kipaumbele cha juu kwa elimu mpaka hapo itakapofikia
mahali kwamba matatizo makubwa yatakapokuwa yamepungua sana.
Hitimisho
Ndugu
Wananchi;
Mungu Ibariki
Tanzania!
Mungu
Ibariki Afrika!
Nashukuru kwa kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment