Monday, March 4, 2013

SHEIKH PONDA ISSA PONDA AKUTWA NA KESI YA KUJIBU



HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salam, imebaini kuwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania,Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49 wana kesi ya kujibu katika mashtaka yote matano yanayowakabili.
Sheikh Ponda na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matano, likiwamo la kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya Sh 59.6 milioni, uchochezi na kuingia kwa jinai katika ardhi inayomilikiwa na kampuni ya Agritanza Ltd kwa nia ya kujimilika isivyo halali.

Akitoa uamuzi juu ya kesi hiyo Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa alisema mahakama imepitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 17 wa upande wa mashtaka, “inaonekana wazi shauri hili linatokana na kipande cha ardhi" alisema Hakimu Nongwa.

Hakimu Nongwa alisema inaonekana wazi kuwa baada ya Bakwata kubadilisha ardhi ya ekari nne zilizopo Chang’ombe Malkazi na 40 za Kampuni ya Agritanza Ltd zilizopo Kisarawe, kuna baadhi ya waislamu hawajaridhika.

Alisema Mahakama haitaujadili kwa undani ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, kwa ajili ya kutatua mambo zaidi, mahakama inatambua umuhimu wa majadiliano hivyo inaona ni vema ikawapa nafasi upande wa utetezi kujitetea.
“Kila mshtakiwa mmoja anatakiwa aseme alikuwa anatafuta nini katika maeneo yale ya Chang’ombe Malkazi.”Alisema Hakimu. 

No comments:

Post a Comment