Mapigano makali yaliyojiri kati ya majeshi ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa kundi la M23 katika kipindi cha masaa 48 yaliyopita, yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 130 karibu na mji wa Goma, ulioko katika jimbo la Kivu Kaskazini.
Hayo yamesemwa na Lambert Mende Omalanga Waziri wa Habari na msemaji wa serikali ya Kongo wakati alipozungumza na waandishi wa habari mjini Kinshasa. Omalanga ameongeza kuwa, mapigano makali yalishuhudiwa katika eneo la Mutaho lililoko umbali wa kilomita 7 kaskazini mwa Goma kati ya vikosi vya jeshi la serikali na waasi na M23, na kwamba hatimaye vikosi vya serikali ya Kinshasa vimefanikiwa kuwaangamiza waasi 120, kuwatia mbaroni waasi 12 na makumi ya wengine kujeruhiwa.
Omalanga ameongeza kuwa, wanajeshi 10 wa serikali pia waliuawa. Inafaa kuashiria hapa kuwa, mwezi Novemba mwaka jana, kundi la waasi wa M23 lilifanikiwa kuuteka mji wa Goma na kuukalia kwa mbavu kwa muda wa siku 10, lakini lililazimika kuondoka baada ya kukabiliwa na mashinikizo makubwa ya nchi za eneo la Ukanda wa Maziwa Makuu ya Afrika.
No comments:
Post a Comment