Tuesday, May 21, 2013

MISAMAHA YA KODI NI JANGA KWA MUSTAKABALI WETU KAMA TAIFA


       By Said Msonga
Misamaha ya kodi imefikia Tsh 1.8 Trilioni kwa mwaka, hizi ni fedha nyingi sana endapo kama zingetumika vema katika miradi ya kimaendeleo. Jana Dr John Pombe Magufuli amesoma bajeti ya Wizara ya Ujenzi yenye jumla ya Tsh 1.2 Trilioni (hivyo misamaha ya kodi ni 150% ya bajeti ya Ujenzi kwa mwaka 2013/14, pia ni 300% ya Bajeti ya Wizara ya Maji 2013/14). Ni nani hasa anayesamehewa matrilioni haya na kwa manufaa gani kwa umma wetu?

Ipo haja sasa tukawa na mfumo makini wa kuchunguza ni kina nani? kwa shughuli zipi? zenye tija gani na umma wanastahili kupewa misamaha hii ya kodi? Inawezekana tukaendelea kulialia kuwa nchi yetu ni masikini lakini tunasahau kuwa huwenda umasikini wetu ni "ukosefu wa viongozi makini" ambao wanaweza kusimamia vema mapato ya nchi na kupanga mipango ya kimaendeleo.

Nakumbuka mwaka 2009 (kama sijakosea) Serikali kwa ushauri wa TRA iliridhia kufuta misamaha ya kodi isiyo na tija kwa mashirika, makampuni na taasisi za kidini ili kuongeza ukusanyaji mapato na kudhibiti mianya ya matumizi mabovu ya fursa ya misamaha ya kodi. Kila mmoja anakumbuka taasisi za dini ndizo zilikuja juu na kumlazimisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kufuta uamuzi wa Serikali ambao ulikuwa umepokelewa kwa mikono miwili na wana taifa hili.

Kama mipango ya Ujenzi wa miundombinu aliyotusomea Dr Magufuli haitakamilika kwa kisingizio cha kuwa na nakisi ya bajeti, kama miradi ya maji mijini na vivijini haitakamilika kwa kisingizio cha nakisi ya bajeti ni wazi kuwa taifa hili tunaongozwa na watu wasio makini na maisha ya watanzania wenziwao, na kwa mnasaba huo viongozi hao watakuwa wamethibitisha kushindwa kwao kiuongozi na wajibu wa wanataifa hili ni kuwachukulia hatua stahiki muda ukiwadia.

Pamoja na hayo ni wakati sasa wa kujua ni kina nani wanaonufaika na misamaha hii ya kodi? Tunakumbuka ripoti ya TRA ilibaini kuwa watu/makampuni/mashiriki/taasisi za dini wanajinufaisha sana na kujineemesha kutokana na misamaha hii ya kodi. LAZIMA tuwe na mfumo maalumu wa kuzifuatilia fedha hizi ili kama zina manufaa yaonekane kuleta athari kwa jamii na pia shughuli za taasisi na mashirika hayo ziwe zinafanyiwa ukaguzi kubaini uhalisia wake badala ya kuyaacha mambo kujiendesha kihobelahobela.

Kama itaonekana inafaa ni vema Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) awe anapitia hesabu za mashirika na taasisi hizi zinazonufaika na misamaha hii (kama baadhi ya wadau wanavyopendekeza) na kama itabainika kuna ubadhirifu basi watakaobainika wafutiwe misamaha na kufikishwa kortini kwa uhujumu wa uchumi.

Ifike mahali Wizara nyeti kama Ujenzi, Afya, Elimu, Kilimo, Maji n.k bajeti zake ziwe zinajitosheleza na mipango yake kukamilika ili kupunguza umasikini kwa watu wetu na kufungua fursa zaidi za wananchi kujiimarisha kiuchumi na kijamii.

Binafsi naamini kama tutajipanga kikamilifu, na tukawa na viongozi makini wenye utu na uzalendo kwa taifa hili ni wazi kuwa tunaweza kutumia vema fursa tulizonazo kujiletea maendeleo na kupunguza utegemezi kwa misaada ya wahisani ambayokwayo imekuwa ikitugharimu kila mara na kutofikia malengo yetu

No comments:

Post a Comment