Padri wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya Machui,
Joseph Monesmo Magamba amemwagiwa tindikali na watu wasiojulikana katika
Mtaa wa Mlandege jana jioni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi,
Haji Hana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba kiongozi huyo
wa dini amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, akiendelea na matibabu
baada ya kujeruhiwa usoni, kifuani na mikononi.
Hana alisema kwamba Padri Magamba (60) alikuwa
akitokea katika duka la huduma za mawasiliano ya mtandao la Shine Shine
saa 10.15 jioni na watu waliommwagia walimtega mlangoni kabla ya kufanya
uhalifu huo na kutoweka kwenye vichochoro vya Mitaa ya Mtendeni na
Mchangani.
Alisema polisi wamestushwa na tukio hilo kwa vile
limetanguliwa na matukio matatu ya kumwagiwa tindikali kwa viongozi wa
dini na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano wa kufanikisha kuwakamata
watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Hili ni tukio la tano kutokea visiwani Zanzibar ambapo Septemba 13
mwaka huu, Sheha wa Shehia ya Tomondo, Wilaya ya Magharibi Unguja,
Mohammed Omar Said (65), alimwagiwa tindikali na mtu asiyejulikana
wakati alipokuwa akichota maji nje ya nyumba yake.Desemba mwaka jana, padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki Zanzibar alipigwa risasi na Februari 17 mwaka huu, padri Evarist Mushi wa kanisa hilo aliuawa kwa kupigwa risasi wakati akienda kuongoza ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Teresia.
Novemba 5, 2012, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, naye alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana wakati akifanya mazoezi katika kiwanja cha Mwanakwerekwe.
Agosti 7 mwaka huu raia wawili wa Uingereza walimwagiwa tindikali kwenye eneo la Mji Mkongwe visiwani Zanzibar "Stone Town".
Wasichana hao wawili wa miaka 18 walikuwa walimu wa kujitolea katika shule moja ya Kanisa la Anglikana visiwani humo.
CHANZO: MWNANCHI/ T. DAIMA
No comments:
Post a Comment