Rais Jakaya Kikwete amesema wale
wote wanaombeza kuhusu utendaji wake, wataona aibu atakapomaliza muhula
wake 2015 huku akiwananga baadhi ya wanaCCM kwa kushindwa kuyaelezea
mafanikio ya Serikali chini ya chama hicho.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme katika mikoa ya Mwanza na Geita unaofadhiliwa na Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC), Rais Kikwete alisema: “Wakati wa kampeni nilibezwa sana, lakini sasa ninawaomba walionibeza kufika vijijini na kuangalia ukamilishaji wa ahadi zangu.
“Nataka waje waone, kwa sasa ninakamilisha
usambazaji wa umeme katika vijiji vyote ili kufikia lengo la Watanzania
asilimi 30 kufikiwa na nishati hiyo. Hadi 2015 umeme utakuwa umesambaa
nchi nzima.
“Serikali yangu itavunja rekodi ya kusambaza umeme
katika vijiji vingi nchini…Tumejenga mtandao wa barabara kwa sasa, hali
yetu ya barabara ni bora Afrika Mashariki, tuliahidi meli Bukoba naomba
niwaeleze kuwa zinakuja, tena siyo moja ni meli mbili.
Septemba 2 mwaka huu, Serikali kupitia Wakala wa
Umeme Vijijini (REA) ilitangaza kuanza kwa awamu ya pili ya usambazaji
wa umeme vijijini, mpango ambao utagharimu Sh881 bilioni na kukamilika
Juni 2015.
Katika utekelezaji wa mradi huo, huduma za jamii
zitakazopewa kipaumbele katika kuunganishiwa umeme ni shule, zahanati,
misikiti, makanisa na visima vya maji.
Mpango huo unatarajiwa kuinufaisha mikoa 24 ya
Tanzania Bara, huku wateja 250,000 wa awali wakiunganishwa pamoja na
kuhusisha kazi ya usambazaji umeme kwenye makao makuu ya wilaya 13
zisizokuwa na umeme.
Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Balozi Ami Mpungwe
alisema tayari mikoa 14 imepata makandarasi na ujenzi wa vituo sita vya
usambazaji umeme, wakati mchakato wa kuwapata wajenzi katika mikoa 13
iliyokosa wakandarasi awali, unaendelea.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment