Wakati magaidi wawili wakiwa wameuawa, Serikali ya Kenya imesema idadi ya watu waliokufa katika tukio la kigaidi kwenye maduka makubwa ya Westgate, Nairobi imefikia 62.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mchana,
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Ole Lenku alisema watu
waliojeruhiwa ni 175 baada ya magaidi hao kuvamia eneo hilo la maduka
tangu Jumamosi iliyopita.
Ole Lenku alisema pia kuwa askari 10 wamejeruhiwa
katika operesheni hiyo inayowahusisha maofisa wa Shirika la Ujasusi la
Israel (Mossad), wale wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).
Alisema askari waliojeruhiwa na raia wanatibiwa katika hospitali mbalimbali za Nairobi.
Magaidi wawili wauawa
Alisema magaidi wawili waliuawa na vikosi vya
usalama huku mapambano yakiendelea. Alisema waasi hao wamebanwa baada ya
vikosi vya ulinzi na usalama kudhibiti sehemu kubwa ya jengo hilo.
Magaidi hao wanaoaminika kuwa wafuasi wa kundi la
Al-Shabaab la Somalia walivamia jengo hilo la ghorofa nne ambalo lina
maduka ya kifahari na kuua, kujeruhi na kuwashikilia wengine mateka.
“Tumeua magaidi wawili na wengine kadhaa
wamejeruhiwa, tutatoa taarifa nyingine baadaye. Hakuna gaidi hata mmoja
ambaye ataondoka,” alisema Ole Lenku na kuongeza: “Ni labda
wajisalimishe au wauawe.”
Alisema magaidi hao wamejaribu kuwasha moto katika
duka la Nakumatt lililopo katika jengo hilo la Westgate ili
kuvichanganya vikosi vya usalama lakini hawakufanikiwa kutokana na
vikosi hivyo kuwa imara.
Ole Lenku alisema kazi ya kupambana na magaidi hao
imechukua muda mrefu kutokana na vikosi vya usalama kufanya jitihada za
kuokoa mateka ambao bado wanashikiliwa.
“Hadi sasa bado hatujui kuna mateka wangapi ndani ya jumba hilo,” alisema Ole Lenku.
Milio ya risasi iliendelea kurindima siku nzima ya jana ndani ya jengo hilo huku askari wengi wakiwa wamelizunguka.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment