RAIS Paul Kagame wa Rwanda amemteua Mtanzania, Profesa Silas Rwakabamba
kuwa Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri
yaliyofanyika Jumatatu iliyopita.
Kabla ya uteuzi huo, Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Taifa cha Rwanda. Ni mmoja wa mawaziri wanaoingiza sura mpya katika Baraza la
Rais Kagame ambalo amelifanyia mabadiliko kwa kuunda wizara nyingine mpya.
Profesa Rwakabamba alikuwa Mtanzania aliyeamua kuchukua uraia wa Rwanda na
alizaliwa katika Kijiji cha Bushagara, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera
Naibu Makamu Mkuu - Taaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Profesa
Makenya Maboko alisema Profesa Rwakabamba alifanya kazi katika chuo hicho na
aliondoka akiwa Mkuu wa Kitivo cha Uhandisi.
“Aliondoka wakati Kagame alipoingia madarakani na alikwenda kuongoza
Taasisi ya Teknolojia ya Kigali (KIST) kabla ya kwenda katika Chuo Kikuu cha
Kigali,” alisema Profesa Maboko.
Msomi huyo alikwenda Rwanda mwaka 1997, baada ya kuombwa na Rais Kagame
ambaye alikwenda UDSM kuwaomba baadhi ya wahadhiri kwenda Kigali kufungua chuo
kikuu katika taifa lake baada ya kumalizika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka
1994.
Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa kwanza wa KIST na kukifanya kuwa
miongoni mwa vyuo bora barani Afrika kwa masuala ya teknolojia jambo
lililomfurahisha Rais Kagame.
Baada ya mafanikio hayo, Rais Kagame alimteua kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Taifa cha Rwanda, Butare ambako pia alijizolea sifa baada ya kusimamia vyema
ujenzi wa mabweni kwa wingi na kiongozi huyo alimtunukia uraia wa nchi hiyo
kama zawadi.
Hata hivyo, Profesa Rwakabamba atakuwa amelazimika kuukana uraia wa
Tanzania kwa kuwa katiba ya nchi hairuhusu uraia wa nchi mbili.