Tuesday, February 12, 2013

MAPIGANO YA KIDINI GEITA YASABABISHA MAUAJI


MCHUNGAJI wa Kanisa la Pentecoste Assemblies of God Tanzania (PAGT) Buseresere, Wilaya ya Chato, Mathayo Kachila (45) amefariki dunia na watu 15 wakijeruhiwa kwa mapanga kufuatia vurugu inayotokana na mgogoro wa bucha.
Tukio hilo lilitokea jana saa 2 asubuhi kwenye Soko la Buseresere baada ya kundi la wananchi kuvamia bucha iliyokuwa na maandishi ya ‘Bwana Yesu Asifiwe, Yesu ni Bwana’, kuwataka waliokuwa wakiuza kuifunga hali iliyozusha vurugu.

Inadaiwa kabla ya kufunguliwa kwa bucha hiyo, Wakristo walifanya mkutano wa Injili Uwanja wa CCM Katoro na kutangaza kuwa, watachinja nyama yao na kuiuza kwenye bucha maalumu.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, wananchi hao wanaodaiwa kuwa waumini wa Kiislamu walikuwa wamechukizwa na kufunguliwa kwa bucha hiyo, ndiyo wakachukua uamuzi wa kwenda kuamuru ifungwe.

“Tulipata taarifa za kufunguliwa kwa bucha hii na tulipofika kuwaomba waache kuuza nyama yao, waligoma na kuendelea kuuza, baada ya kuona hilo wafuasi wa Dini ya Kiislamu walikimbilia msikitini na kuunda kikosi cha kupambana nao,” alisema Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Wilaya ya Chato, Yusuf Idd.
Alisema licha ya kuwasihi hawakumsikiliza, waliamua kwenda kupambana.

Katika vurugu hizo, duka la Idd lilivunjwa na kuporwa simu na fedha, huku pikipiki mbili ambazo hazijafahamika wamiliki zilichomwa moto.
Katika vurugu hizo nyama ndani ya bucha hiyo ilimwagiwa maji, ikiwamo kuharibiwa kwa madirisha na milango yake.

Licha ya majeruhi kutajwa kuwa 15, waliotibiwa Kituo cha Afya Buseresere na kuruhusiwa ni Abdallah Shaaban (25), Abubakar Shaaban (27), Faruk Shaaban (14), Kassim Almasi (23), Yusuf Shaaban (18), Bilal Hassan na Abdallah Ibrahim.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Geita, Dk John Lumona alisema majeruhi wengine waliofikishwa ni Yasin Rajabu (56), Said Taompangaze (47), Masoud Idd (21), Ramadhan Pastory (36), Haruna Rashid (61) na Sadiq Yahya (40), ambaye hali yake ameieleza kuwa mbaya na alipelekwa Hospitali ya Rufani Bugando.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geira, Paul Katabago alithibitisha kutokea kwa tukio hilo huku Mkuu wa Wilaya ya Chato, Rodrick Mpogolo aliwataka wananchi kutulia kwa vile suala hilo linashughulikiwa na serikali na litapatiwa ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment