Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA
(Bara), Zitto Kabwe amesema ubadhiliu wa shilingi trilioni 1 na mkataba wa ujenzi wa bomba
ka mafuta Mtwara ni chanzo cha kufutwa kwa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya uma
(POAC)
Akizungumza katika mikutano wa
hadhara jijini Dar es Salam ikiwa ni muendelezo wa mchakamchaka wa chama hicho ulioanzia bungeni wa kutaka
hoja zake zisikilizwe baada ya kutupiliwa mbali kimizengwe bungeni.
Zitto ametaja sababu ya kufutwa kwa
kamati hiyo kuwa ni utendaji wa kamati hiyo uliogundua matumizi ya zaidi ya Sh1
trilioni kutoka kwenye mifuko ya pensheni zilizotumika katika kampeni za CCM,
na ujenzi wa vyuo vikuu vya Dodoma, Hombolo na Chuo Kikuu cha Arusha Nelson
Mandela.
“Spika lazima ajue kwamba mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la Wananchi liitwalo Bunge. Anna Makinda lazima adhibitiwe, vinginevyo nchi yetu itaumia,” anasema Zitto.
Zitto aligusia pia sakata la Mtwara akisema kamati iliyofutwa ililitaka Shirika la Maendeleo ya Mafuta (TPDC) kuonyesha mkataba wa ujenzi wa bomba la mafuta, wakaahidi kuupeleka ifikapo Aprili mwaka huu.
“Tulipowataka TPDC watuletee mkataba wa ujenzi wa bomba la gesi wakasema uko wizarani. Katibu Mkuu ambaye anapaswa kwenda kujieleza kwenye Kamati ya Nishati na Madini hakwenda kwa kuwa kamati hiyo pia imefutwa. TPDC wakasema watauleta Aprili. Ndiyo hivyo kamati yetu nayo imefutwa.”
Wabunge wa upinzani waliowasilisha hoja zao ni pamoja na Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia aliyetaka mfumo wa elimu nchini ufumuliwe au kuboreshwa, kero ya maji jijini Dar es Salaam iliyotolewa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika
Hali hiyo ilizua vurugu na matokeo yake hoja nyingine binafsi za wabunge, ikiwamo ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari aliyetaka kujadiliwa kwa mwenendo wa Baraza la Mitihani la Taifa na jinsi linavyoathiri mfumo wa elimu nchini, ziliahirishwa kwa muda usiojulikana.
Mbali na kuzitupilia mbali hoja hizo, Bunge hilo lilimalizika likiifuta Kamati ya Bunge ya Mashirika ya umma iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Katika mkutano wa hadhara, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Zitto Kabwe anasema Spika wa Bunge, Anna Makinda ameshindwa kuwajibika na hivyo anapaswa kung’olewa kutokana na kutaka kuirudisha nchi kwenye kipindi cha kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu (Epa).
Zitto aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, anasema imefutwa kwa mbinu za CCM kuzima sauti ya wabunge wa upinzani wanaozungumzia maslahi ya wananchi.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment