Tuesday, April 9, 2013

WATU 32 WAPOTEZA MAISHA KATIKA TETEMEKO LA ARDHI IRAN


Jengo lililoharibiwa na zilizala eneo la Kaki kusini mwa Iran Aprili 9 2013

Tetemeko la ardhi  lenye nguvu ya 6.1 kwenye kipimo cha Richter limetikisa eneo la Kaki karibu mji wa Bushehr kusini mwa Iran. Shirika la Habari la Fars limesema  watu 32 wamepoteza maisha na wengine  850 kujeruhiwa katika tetemeko hilo.

Taasisi ya Kupimatetemeko ya  Iran imesema  tetemeko hilo limejiri leo Jumanne alasiri huko Kaki kilomita tisini kusini mwa Bushehr na kina chake kilikuwa kilomita 12 ndani ya ardhi. Pia limehisika katika nchi za Ghuba ya Uajemi za Kuwait, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Kituo cha Kuzalisha Nishati ya Nyuklia cha Bushehr hakikuharibiwa hata kidogo na tetemeko hilo. Shirika la Urusi la Atomstroyexport ambalo limejenga kituo hicho cha nyuklia limetoa taarifa na kusema kinu cha  nyuklia cha Bushehr kiko katika hali ya kawaida. Iran  iko katika eneo ambalo hukumbwa na mitetemeko ya ardhi mara kwa mara.

CHANZO: IDHAA YA KISWAHILI-TEHRAN

No comments:

Post a Comment