Wednesday, April 24, 2013

UGONJWA WA KIMETA WAINGIA NCHINI, WAUA MTU MMOJA


Ugonjwa wa kimeta umelipuka katika Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro na kusababisha kifo cha mtu mmoja na mifugo kadhaa. Kutokana na hali hiyo, wakazi 386 katika kijiji cha Kibaoni kata ya Nanjara Reha wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, wamepatiwa chanjo kufuatia ugonjwa huo. 

Akizungumza na NIPASHE, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Judathadeus Mboya, alisema Aprili 5, mwaka huu katika Kata ya Nanjara Reha ng’ombe mmoja wa Afisa Mtendaji wa kata ya Ubetu Kahe, Peter Kavishe, aliugua na baada ya kuzidiwa mmiliki wake aliichinja na kuiuza nyama kwa bei nafuu katika kijiwe kwa Mafungu.
Mboye alisema Aprili 15 mwaka huu, Ofisa huyo ambaye aliugua na alizidiwa kutokana na ugonjwa wa kutokewa na  malengelenge makubwa meusi na kukimbizwa katika hospitali ya Huruma. Mboya alisema usiku wa kuamkia Aprili 17, mwaka huu Kavishe alifariki dunia.
Mkurugenzi huyo lifafanua kuwa uongozi wa hospitali hiyo alipokuwa amelazwa Kavishe, baada ya kuchukuwa vipimo walishindwa kuvibaini kwa haraka na kuvipeleka katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na kubaini kuwa ni ugonjwa wa kimeta.
 “Siku hiyo ya tarehe 17, mgonjwa mwingine ambaye alikula nyama hiyo alilazwa katika hospitali ya Huruma na bado anaendelea na matibabu,” alisema Mboya na kuongeza:
“Halmashauri imejitahidi kutoa chanjo kwa watu waliokula nyama na kufikia Aprili 20, mwaka huu watu waliopatiwa chanjo wamefikia 386.”
Hata hivyo, Mboya alisema hadi kufikia juzi idadi rasmi ya mifugo waliokufa kutokana na ugonjwa huo haikujulikana. 
Naye Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Rombo, Frank Mwanri, alimtaja bakteria ambaye huambukia ugonjwa huo kuwa ni Basilus anthrax na dalili za ugonjwa huo ni mifugo kutoa damu isiyoganda katika maeneo yote yenye uwazi.  Mwanri aliongeza kuwa pia kimeta huenea kwa njia ya damu kwa kushika damu au nyama ya mfugo ambao tayari umeathirika na ugonjwa huo. Alisema chanjo kwa ajili ya mifugo ilitarajiwa kuanza rasmi jana wilayani humo.
“Wananchi wote wilayani Rombo, chanjo itaanza rasmi kesho (jana), hivyo tujitokeze kwa wingi ili kupata chanjo ya ugonjwa huu na kuepusha madhara ambayo yanaweza kujitokeza na hata maafa kama tusipoangalia,” alisema Mwanri.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment