Tuesday, November 26, 2013

JAMII YATAKIWA KUTUMIA NAFASI ZILIZOPO KUPAMBANA NA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE



Na Butije Hamisi- Mwanza

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Ernest Mangu Ameitaka jamii na kila mtu kutumia nafasi alonayo kuzuia ukatili wa kijinsia ili kuboresha afya ya jamii.
Ameyasema hayo katika uzinduzi wa siku 16 za kupambana na ukatili dhidi ya wanawake uliofanyika jana katika viwanja vya line polisi Mabatini jijini Mwanza.
Kamanda Mangu amesema kanda ya ziwa inaongoza kwa matukio ya kikatili nchini, hivyo watu wote hawana budi kuamka kupambana na ukatili huo.
“Uwepo wa matukio hayo unaleta haja ya walio katika nafasi kusimama na kuzuia vitendo vya ukatili” alisema kamanda Mangu
Kamanda mangu amesema mkoani mwanza mpaka sasa matukio ya mauaji ya kishirikina yamefikia 40 na watu 44 wakipoteza maisha katika matukio hayo wanawake wakiwa ni 34 na wanaume 10 tu. Huku watuhumiwa 133 wakishikiliwa na jeshi la polisi.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi wa shirika la KIVULINI Bw. Ramadhan Masele  amesema kampeni hiyo ya siku 16 inalenga kuamsha ari kwa watanzania kupambana na ukatili wa kijinsia hususan kwa wanawake na kauli mbiu ya kampeni hiyo ni “Funguka ! Tumia mamlaka yako, zuia ukatili wa kijinsia, kuboresha afya ya jamii.
Bw. Masele amebainisha kuwa kukosekana kwa sheria maalumu inayohusika na ukatili wa kijinsia, mitazamo hasi ya jamii dhidi ya wanawake, ukosefu wa huduma bora za afya na vitisho kwa wahanga wa ukatili ni baadhi ya changamoto zinazo wakabili katika harakati za kupambana na ukatili wa kijinsia.
Pia Diwani wa kata ya Mbugani Bw. Hashim Hassan Kijuu ameitaka jamii kushirikana katika ngazi zote toka familia, mtaa mpaka taifa kupambana dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Shirika la KIVULINI limekuwa likendesha harakati za kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto na siku ya November 25 ya kila mwaka ni siku ya kimataifa ya kupambana na ukatili dhidi ya wanawake duniani.

No comments:

Post a Comment