Wednesday, November 27, 2013

KAIRUKI ATAKA USHIRIKIANO KUUKABILI UNYANYASAJI

Washiriki mbalimbali wa maendeleo na wadau wa masuala ya jinsia wametakiwa kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia vinafikia tamati.

Rai hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki wakati akizindua siku 16 za kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Sambamba na uzinduzi huo Kairuki alizindua pia mfumo wa utoaji wa huduma kwa mfumo wa One Stop Center ambao unajumuisha huduma zote muhimu kwa watakaokutana na ukatili wa kijinsia kama vile polisi, afya na ustawi wa  jamii kutolewa sehemu moja.
Alisema licha ya kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikiongezeka kila kukicha, ni asilimia 4 tu ya kesi hizo ndiyo huripotiwa katika vyombo vya sheria hali inayochangia wahusika kuendelea kuwa huru mitaani.
“Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha vitendo hivi vinatokomezwa, lakini wanawake ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo wamekuwa wakinyanyasika hawakimbilii kutafuta msaada wa kisheria” alisema Kairuki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF), Naomi Kaihura alisema licha ya kuwepo kwa jitihada mbalimbali za kupinga vita vitendo vya ukatili, changamoto kubwa inabaki katika upatikanaji wa fomu za polisi ambazo hutoa kibali kwa muathirika kupata matibabu.
Alisema hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachangia waathirika kupoteza maisha na wengine kukata tamaa ya kutoa ripoti kuhusiana na ukatili waliofanyiwa.
“Ukiritimba katika upatikanaji wa PF3 ni changamoto kubwa hali inayosababisha  waathirika kupoteza maisha hata kabla hawajapata matibabu,” alisema.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment