Monday, December 16, 2013

MSIBA WA BARABARA KIKWAZO CHA USTAWI WA TAIFA, WACHANGIA KUZOROTA KWA SEKTA ZINGINE ZA MAENDELEO


By Butije Hamisi
Nilipita Maeneo mengi! Badhi yalikuwa na mvua, mengine jua kali na mengine yalikuwa na hali ya mawingu na mvua za rasharasha. Nilipita ktk mlima Sekenke sikujua hali ilikuwaje kwani nilikuwa nimesinzia na sasa nipo Dar es Salaam, Tanzania.

Nikiwa safarini nilipigwa na bumbuwazi na kujiuliza HIVI BARABARA ZETU HUWA ZINA EXPIRE (zinakwisha muda wa matumizi yake) baada ya muda gani? Hivi huwa zina expire ndani ya mwaka mmoja? maana kila ukisafiri toka Mwanza/Kigoma kwenda Dar. lazima utakuta sehemu wanatengeneza barabara. Smehemu iliyotengenezwa miezi michache iliyopita utakuta tena inatengenezwa upya au kufanyiwa marekebisho.

Sasa nabaki najiuliza huwa zinatengenezwa zitumike ndani ya mwaka mmoja kasha zitengenezwe tena? Ukiangalia barabara ya kutoka Morogoro to Dodoma upande unaopita gari kutoka Moro to Dom umetitia. Ninajiuliza barabara haina kiwango? au inapitisha vitu vizito zaidi ya uwezo wake? Jijini Dar babara ya Mandela imekuwa ilikarabatiwa kila mara na baada ya muda mfupi inaharibika.
Swali kwa serikali na wadau, Kama tatizo ni mizigo mizito je suluhisho hamlijui? Miaka kadhaa kabla ya shirika la reli T. kubinafsishwa kwa waliojiita wawekezaji ambao walishidwa kuliendesha shirika mizigo mingi ilikuwa ikisafirishwa kwa njia ya reli iweje ishindikane leo? Hivi taifa/Serikali imeshindwa kutumia ipasavyo rasilimali tulizonazo kuboresha reli ili kuokoa maisha ya barabara zetu zinazoendelea kuteketea kila kukicha katika tanuri la malori?

Ni wazi kuwa barabara zetu zimekuwa zikitengenezwa kwa fedha nyinggi ambazo hutoka kwa Wasakatonge/Walipakodi ambao ambao wengi wao ni wananchi wa tabaka la chini na kati maana wenyenavyo maranyingi wamekuwa wakisamehewa kodi kwenye biashara zao. Fedha zingine zimekuwa zikipatikana kama mikopo toka kwa "Wakoloni Mamboleo" ambapo Msakatonge ndiye atakakuja kulipa mkopo huo katika njia zitakazoainishwa na serikali.

Kwa kutambua kuwa barabara hizo zinagharimu fedha nyingi zimekuwa zikiharibika kwa muda mfupi kutokana na malori yanayopita yakiwa yamesheheni mizigo zaidi ya kiwango kinachotakiwa. Hapa Napata kigugumizi kidogo! nawaza na kujiuliza, Hivi serikali yetu imekosa "Meno" ya kung'ata malori yote yanayozidisha uzito? Hivi tuliowapa mamlaka ya kusimamia sharia za nchi yetu wamekosa huruma na kuzuia machozi yanayobubujika kutoka katika barabara zetu?

Ninaelewa kuwa lengo kuu la serikali thabiti kokote duniani ni kuboresha maisha ya wananchi wake katika Nyanja zote ikiwemo kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni. Lakini hapa Napata shaka kidogo kama serikali yetu inaweza kulifikia lengo hilo kwa wakati. Kuboresha barabara ni hatua muhimu ya kulifikia lengo hilo lakini kila inapoboresha zinaharibila kwa muda mfupi hku sababu za uharibifu huo wakiwa wanazijua.

Niwazi kuwa kama uharibifu huo unaogharimu na kupoteza mabilioni ya shilingi ungelikomeshwa fedha hizo zingeelekezwa katika kuokoa maisha ya wajawazito na watoto wachanga wanaopoteza maisha kila kukichakutokana na uduni wa huduma za afya. Fedha hizo zingetumika katika kutoa zuruku kwa wakulima, pia zingeliwekezwa katika sekta ya viwanda nchini ili kukuza uchumi wa taifa na wananchi wake. pia zingesaidia kupunguza mfumko wa bei za bidhaa ili kuleta nafuu ya maisha kwa watanzania wa hali ya chini ambao ndio wengi.

Ninaamini  kuwa kama uharibifu huo ukidhibitiwa fedha zinazoelekezwa huko zitasaidia kuwekeza vya kutosha katika sekta ya elimu kwa kujenga maabara za kisasa, kununua vitabu vya kutosha, na vifaa vya kufundishia ili kuboresha elimu yet, pia zingesaidia kuboresha maslahi ya walimu ili kuwafanya wasomi wengi kujiona ni wa fahari na wamaana kuwa mwalimu kwani ukienda katika shule za sekondari, vyuo vya kati na vyuo vya elimu ya juu wanafunzi wengi wamekuwa hawataki kusomea ualimu na baadhi yao wamekuwa wakienda kwenye ualimu pindi anapoona hana chaguo linguine. Na hata wale waliosomea ualimu bado baadhi yao hawataki kuwa walimu na kukimbilia katika sekta zingine kufuata maslahi na mazingira bora ya kazi.

Nachukua fursa hii kuikumbusha serikali kutekeleza wajibu wa kuboresha maisha na kuinua uchumi wa watanzania, kwa kuanzia ikomeshe uharibifu na msiba wa barabara unaoendelea nchini kwa kuzuia usafirishaji wa mizigo na abiria kwa kuzidisha kiwango kinanchotakiwa kwa viwango vya barabara zetu.

Hili likifanikiwa fedhaambazo zingeelekezwa katika kukarabati barabara hizo zitaelekezwa kwenye ujenzi wa barabara mpya na kwenye sekta zingine kama afya, elimu, viwanda na kilimo ili kuboresha maisha ya watanzania hususana wananchi wa tabaka la chini.


Wahenga walisema mchelea mwana kulia hulia mwenyewe, tusipochukua hatua stahiki na kwa wakati, tusipotumia rasilimali zetu ipasavyo tutaendelea kupiga maktaimu na hatutofika malengo tuliyojipangia katika kujiletea maendeleo na kuboresha maisha ya watanzania wote. Msiba wa barabara ni kikwazo cha ustawi wa taifa.

Maoni +255752231172

No comments:

Post a Comment