Saturday, November 17, 2012

ISRAEL YAFANYA MAUAJI HUKO GHAZA


 

 SOURCE: Idhaa ya Kiswahili ya Tehran

Jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel katika duru mpya ya mashambulizi yake huko Ghaza ambayo yalianza Jumatano iliyopita zimekuwa na maafa ya kutisha sawa na mashambulizi mengine ya utawala huo, kwa kadiri kwamba hadi sasa mamia ya Wapalestina wameuliwa shahidi na kujeruhiwa, wengi wao wakiwa ni watoto wadogo, wanawake na wazee.
Jinai kubwa za utawala wa Kizayuni katika siku kadhaa zilizopita zimewatia wasiwasi mkubwa walimwengu. Ripoti za mashirika mbalimbali ya kimataifa kuhusu takwimu za watu waliouliwa katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika siku kadhaa zilizopita huko Ghaza zinazungumzia maafa makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika duru hii mpya ya hujuma ya Israel huko Ukanda wa Ghaza.
Taarifa ya Mfuko wa Watoto wa Kimataifa (Unicef) imeeleza kuwa makumi ya watoto wa Kipalestina wameuliwa au kujeruhiwa katika mashambulizi yanayofanywa sasa na utawala wa Kizayuni huko Ghaza. Hii ni katika hali ambayo idadi ya Wapalestina wanaouliwa shahidi katika mashambulizi hayo ya Israel hususan watoto wadogo inaongezeka.
Weledi wengi wa masuala ya kisheria wamesema baada ya kushuhudia na kutathmini hali ya mambo ya Ghaza kuwa hatua ya Israel ya kuendelea kuwauwa kwa umati Wapalestina ni ushahidi wa wazi wa jinai dhidi ya binadamu. Katika mazingira hayo fikra za walio wengi zinataraji kuwa taasisi za kimataifa zitachukua hatua haraka iwezekanavyo kusimamisha jinai hizo za utawala wa Kizayuni na mauaji makubwa yanayofanywa dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Palestina. Hii ni katika hali ambayo taasisi za kimataifa zimeendelea kukaa kimya mbele ya jinai hizo na utawala wa Israel, suala ambalo limeupa utawala huo kiburi cha kuendeleza jinai na mauaji yake huko Ghaza.
Habari zinasema kuwa utawala wa Kizayuni unajiandaa kufanya oparesheni kubwa ya nchi kavu huko Ghaza na katika fremu hiyo Israel tayari imetuma vikosi na zana nzito za kijeshi katika mipaka ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Serikali za Magharibi ambazo zinaendeleza kuuunga mkono utawala haramu wa Israel zimekosolewa vikali na walimwengu na kutambuliwa kuwa ni washirika wakuu wa Israel katika jinai hizo. 
Utawala wa Kizayuni umeshadidisha jinai zake huko Ghaza ili kutimiza malengo yake makuu ambayo moja kati ya hayo ni kujionyesha kuwa na nguvu kubwa na kuzusha hofu na wasiwasi ili kuwalazimisha Wapalestina wasalimu amri mbele ya siasa zake za kujitanua katika ardhi za Palestina. Israel ambayo mwaka 2005 ilipata pigo kubwa mbele ya muqawama wa wananchi wa Palestina na kulazimika kuondoka Ghaza kwa madhila hivi sasa inatumia njia mbalimbali ili kulikalia tena eneo hilo. Mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka 2008, Israel ilianzisha vita vya siku 22 dhidi ya Ghaza kwa uungaji mkono wa Marekani lengo likiwa ni kulikalia tena kwa mabavu eneo hilo. Hata hivyo katika vita hivyo vya siku 22 ambayo vilimalizika mwanzoni mwaka mwaka 2009, utawala wa Kizayuni ulishindwa kufikia malengo yake haramu licha ya kutenda jinai kubwa dhidi ya wananchi wa Palestina na kuwauwa shahidi maelfu ya raia hao kutokana mapambano makubwa ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza.
Kwa hali yoyote ile kushadidi mashambulizi na ukatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Gaza kumedhihirisha tena sura halisi ya ugaidi, kupenda vita, ukatili na mauaji ya utawala huo jambo ambalo limekabiliwa na radiamali kali ya fikra za walio wengi duniani. Maandamano makubwa yanayofanyika katika pembe mbalimbali duniani kwa ajili ya kuulaani utawala haramu wa Israel yanadhihirisha hasira kubwa za waliwengu kwa utawala huo unaotenda jinai za kutisha dhidi ya raia wasio na ulinzi wala hatia wa Ukanda wa Ghaza.

No comments:

Post a Comment