Friday, December 20, 2013

RAIS KIKWETE AKUBALI KUFUTWA KODI YA LAINI ZA SIMU, ASAINI HATI YA DHARURA KUFANYIWA MAREKEBISHO MUSWADA WA FEDHA WA 2013

http://tanganyikaone.blogspot.com
By Butije Hamisi- Dar es Salam

Rais wa  jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Jakaya Kikwete amesaini hati ya dharura (Certificate of Urgency)  kufuta kodi ya Tsh. 1000 kwa mwezi kwa kila laini ya simu iliyopitishwa na Bunge na kuwekwa kwenye bajeti ya 2013/2014.

Kufuatia hatua hiyo Bunge limepelekewa taarifa hiyo na kulichukua kama dharura ili Muswada wa Fedha wa Mwaka 2013 ufanyiwe marekebisho ya kuondoa tozo ya kodi kwa kadi za simu..

Bunge la Bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2012/13 lilipitisha kodi ya Sh1,000 kwa kila kadi ya simu, hatua ambayo ilipingwa na wabunge wengi.
Akithibitisha utiaji saini huo Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema jana kuwa Rais Kikwete alitia saini hati hiyo juma hili.
“Muheshimiwa Rais ametia saini hati ya dharura kufanyika marekebisho kwa muswada wa fedha wa mwaka 2013 kuondoa tozo ya kodi kwa laini za simu” alisema Makamba

Makamba alisema suala la muswada huo kurudishwa bungeni linategemea na ratiba huku akisisitiza kuwa licha ya Bunge kupitisha muswada huo tangu Julai, mwaka huu, bado kodi hizo zilikuwa hazijaanza kutozwa.
Kufuatia kodi hiyo kutoungwa mkono wa wananchi wengi pamoja na wabunge, Julai 23, mwaka huu, Rais Kikwete aliagiza kukutana na mamlaka zinazohusika na kodi na mawasiliano pamoja na kampuni za simu za mikononi ili kutafuta suluhisho la mgogoro huo wa kodi.
Rais Kikwete Alisema lengo kuu la kukutana huko lilikuwa ni kupendekeza jinsi ya kuziba pengo la Sh178 bilioni ambazo zitapotea katika bajeti iwapo kodi hiyo itafutwa
Alitoa kauli hiyo alipokutana na viongozi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia na wawakilishi wa kampuni za simu za TTCL, Airtel, Vodacom, Tigo na Zantel, Ikulu, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment