Friday, May 16, 2014

DIVISION 4 STOP KUSOMEA UALIMU; WANAFUNZI WATAPEWA MKOPO BILA KUUREJESHA

Serikali imesema ili kukabiliana na tatizo la kuwa na walimu waliofeli mitihani ya sekondari kuanzia mwaka huu itaanza kuwasomesha bure wanafunzi waliofaulu, wanaotaka kwenda kusomea shahada ya elimu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Ulimwengu ya Ufuatiliaji wa Elimu kwa wote iliyoandaliwa na Shirila la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi (Unesco), Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alisema kuanzia sasa wanafunzi waliopata daraja la nne hawataruhusiwa kusomea ualimu.
Alisema ili kuwa na walimu wenye uwezo mkubwa wa kitaaluma na kuondokana na dhana kuwa wanaokwenda kusomea kozi hiyo wameshindwa kupata nafasi sehemu nyingine, wanafunzi waliofaulu watapewa mkopo na Serikali na hawataulipa.
“Ukipata daraja hilo ni kwamba hakuna nafasi ya kujifunza ualimu,” alisema na kuongeza kuwa wanafunzi watakaopata daraja la tatu watapewa mkopo, lakini wao watalazimika kuulipia.
Pia ripoti hiyo iliyoangalia namna mafunzo ya elimu yanavyotolewa imebainisha kuwa walimu wa Tanzania wanaongoza kwa utoro kazini katika Ukanda wa Afrika Mashariki jambo lililochangia wanafunzi kufanya vibaya kwenye matokeo yao ya mitihani.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Profesa Galabawa alisema kuna upungufu wa walimu wenye sifa za kufundisha huku taasisi zinazosimamia elimu zikishindwa kukabiliana na tatizo hilo.
Alisema iwapo Serikali inataka kuwa na walimu wenye sifa zinazotakiwa, italazimika kuwa na Dola 335 milioni (Sh536 bilioni) ambazo ni sawa na asilimia 23 ya fedha yote ya bajeti ya wizara ya elimu mwaka 2011 na kwamba Serikali ibadili utaratibu uliopo sasa wa kutoa elimu.

No comments:

Post a Comment