Friday, November 1, 2013

MGOMO WA MADAKTARI WALIOKO MAFUNZONI WANUKIA: BARUA YA WAZI KWA WAZIRI WA AFYA, Mh.Dr. Hussein Mwinyi

BARUA YA WAZI KWA WAZIRI WA AFYA,
Mh.Dr. Hussein Mwinyi


Kwa heshima kubwa, Sisi madaktari na wafamasia tuliopo mafunzoni (Internship) katika hospitali za mikoani tofauti na Muhimbili tunapenda kukutaarifu Mh.Waziri wa Afya,kwamba kumekuwepo na matatizo katika malipo ya posho tunazolipwa kila mwezi.Matatizo hayo ni kuwepo kwa tofauti ya malipo kati ya wale wanaofanya mafunzo ya vitendo katika Hospitali ya Muhimbili na wale wanaofanyia hospitali zilizopo mikoani na tofauti na Muhimbili.

Wakati wenzetu wa Muhimbili wanalipwa 100%,yaani 1,225,000/= kwa madaktari na 994,000/= kwa wafamasia,sisi wa mikoani na nje ya Muhimbili tunalipwa 80% yaani 980,000/= kwa madaktari na 795,200/= kwa wafamasia.
Tumejaribu kufuatilia tofauti hiyo kuanzia mwezi julai lakini hatujapata jibu linaloeleweka kwani ilidaiwa kwamba kulikuwa na makosa ya kiutendaji yalifanyika lakini kwa bahati mbaya mpaka leo tunakuandikia barua hii bado tatizo hilo linaendelea.

Kwa barua hii,tunaomba majibu yaliyokamilika na sahihi kutoka kwako Waziri wa Afya na kwamba tunajiandaa kugoma endapo ufumbuzi wa tatizo hilo hautafanyika kwa wakati kwa sababu hatua ya kutofautisha malipo siyo tu ya unyanyasaji lakini pia ni ya kibaguzi na inavunja katiba yetu ya nchi.
Ni matumaini yetu kwamba madai haya yatafanyiwa kazi ipasavyo na hatimaye kupewa stahiki zetu kama ilivyo kwa wenzetu wa Muhimbili.


NAKALA· Chama cha madakatari Tanzania· Baraza la Famasi· Gazeti la Mwananchi· IPP media· Freemedia Group · Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)

No comments:

Post a Comment