Sunday, November 3, 2013

LEMA: UNAFIKI WA ZITTO KABWE NA SUALA LA POSHO

UNAFIKI WA ZITTO KABWE NA SUALA LA POSHO – LEMA

Kama nilivyosema jana kuwa leo kabla ya saa nane mchana nitaweka wazi unafiki wa Zitto katika suala la posho , suala ambalo halihitaji vikao vya Chama kulijadili isipokuwa vyombo vya habari na hususani mitandao ya kijamii kama yeye anavyofanya na kujaribu kupotosha ukweli na kutafuta sifa ambazo kimsingi hana.

CHADEMA wakati inaamua kulijadili suala hili la posho , msingi wake mkuu ulikuwa kama ifuatavyo :

1)
CHADEMA iliona na kutambua ubadhirifu unaofanyika kupitia kivuli cha posho katika Taasisi za Umma na Serikali na sio Bunge pekee , hivyo CHADEMA ikapendekeza mishahara ipandishwe na posho zisizo za lazima ziondolewe ili kuondoa mwanya wa ubadhirifu wa fedha za Umma .Huu ndio uliokuwa msimamo wetu .


Kulikuwa na msingi mkuu ambao ungekuwa na faida kubwa kwa Nchi na Watu wake lakini kabla msimamo huu haujawekwa hadharani na kutafsiriwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni , Zitto Kabwe tayari alishatoka katika vyombo vya habari ni kujipambanua kuwa yeye hataki posho na wala hatachukua posho , na hapa vyombo vya habari vilichukua jambo hili kama hoja yake binafsi na huku mantiki ya hoja kamili ikipotea . ( Mantiki ilikuwa ni kuondoa posho zisizo za msingi kwa Watumishi wote wa Umma na kuboresha masilahi yao kwa maana ya mishahara )

Lengo kubwa la Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA ni kupigania masilahi bora ya Watumishi wa Umma na Sekta binafsi katika Nchi hii . Msingi wa CHADEMA ulikuwa na maana pevu kwani tulijua kama mishahara ikiongezwa itampa fursa Mtumishi kuwa na Maisha bora leo na hata baadaye kwa mafao bora baada ya utumishi wake kazini . Lakini ingekuwa rahisi pia kwa Mtumishi kuwa na uwezo mkubwa wa kutafuta mikopo kwa ajili ya maendeleo kwani Mabenki yanatoa mikopo kupitia mishahara ya Watumishi . Ikumbukwe kwamba , mtumishi mwenye mshahara mzuri anakuwa na fursa ya kupata mkopo mkubwa ambao utatatua matatizo yake mengi . Kwa hiyo msingi wa kutaka posho zisizo na msingi ziondolewe ilikuwa ni mkakati wa CHADEMA kuboresha masilahi ya Umma kupitia mishahara .

Niliposema Mh Zitto ni mnafiki kuhusu suala hili , nilikuwa na maana ifuatavyo :


Kwamba , sio kweli kuwa kukataa posho ni uzalendo na hata ingekuwa ni uzalendo Zitto sio mzalendo katika suala hili la fedha na maisha yake . Aliposema hatachukua posho Wananchi wengi walimuona ni shujaa , ushujaa ambao hana katika jambo hili . Nasema hivi kwa sababu , Wakati Zitto anakataa posho ya kikao ya shilingi sabini elfu ( 70,000 /=) kwa siku ambayo ni sawa na shilingi takribani milioni kumi na mbili kwa vikao vyote vya Bunge kwa Mwaka , Zitto huyo huyo , anapokea posho ya kikao kati ya shilingi laki saba hadi milioni moja kwa kikao kimoja katika vikao vinvyofanywa na mashirika mbali mbali hususani Mashirika ya hifadhi za Jamii . Maana yake ni kwamba kama anapokea laki saba kwa siku na mashirika haya kwa ujumla wake yakafanya vikao ishirini tu kwa mwaka na mara nyingi Zitto kama Mwenyekiti wa PAC huwa anapata mwaliko wa kuhudhuria vikao hivi , basi atakuwa akipata posho ya kikao takribani ya shilingi milioni kumi na nne mpaka milioni ishirini kwa vikao visivyozidi ishirini , wakati kule juu amekataa posho ya shilingi milioni takribani kumi na mbili kwa vikao vya siku takribani mia moja na themanini ambayo ni miezi sita .

Ikiwa vikao hivyo vya mashirika anayohudhuria Zitto kama Mwenyekiti wa PAC ni vya siku mia moja themanini kama ilivyo kwa vikao vya Bunge basi Zitto atakuwa anapokea posho kati ya ya shilingi milioni mia moja na ishirini na sita elfu na laki sita ( 126,600,000) na milioni mia moja na themanini ( 180,000,000) . Na hapa naomba kutaja masilahi yangu katika hili kwani Wabunge wa kawaida ikiwa wakialikwa katika vikao hivyo huwa wanalipwa shilingi laki tano kwa kikao kwa siku . Mimi nimewahi kuhudhuria vikao hivyo mara mbili na nikalipwa hivyo pamoja na chai na chakula cha mchana . Tofauti na Mwenyekiti wa Kamati ya PAC yeye pamoja na posho anayochukua ( 700,000 - 1,000,000) hupewa mafuta ya gari au tiketi ya ndege yamkutoa alipo na kumrudisha na kukodiwa Hoteli yenye hadhi ya nyota nne mpaka tano ambayo kwa siku . Hotel hiyo hulipiwa kati ya dola za Marekani mia moja mpaka dola mia sita kwa siku .

Ø JE MTU HUYU ANAYEPINGA POSHO YA ELFU SABINI YA KIKAO CHA BUNGE AMBACHO MSINGI WAKE NI UWAKILISHI WA WANANCHI NA KUKUMBATIA POSHO YA YA SHILINGI LAKI SABA HADI MILIONI MOJA YA MASHIRIKA AMBAYO MSINGI WAKE PENGINE NI KUWAZIBA MIDOMO WENYEVITI WA KAMATI ZA BUNGE KATIKA MASHIRIKA HAYO NDIYO UZALENDO ? HUU NI UNAFIKI WAKUTAKA SIFA AMBAZO HAZINA MSINGI.

Lakini huyu Zitto anatoka Jimbo lenye Umasikini mkubwa ambapo naamini kuwa kuna wahitaji wengi kama yatima , wajane , wazee , na wasiojiweza kwa namna mbali mbali , kama yeye ni mzalendo kwa nini asingetumia malipo yake hayo halali kuwasaidia hao ndugu na Jamaa na Wapiga kura wake ?

Ø NI NA WASI WASI NA UZALENDO ANAOUHUBIRI ZITTO , NA AMEPOTEZA MWELEKEO WA HOJA YA MSINGI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI INAYOONGOZWA NA CHADEMA JUU YA FIKRA SAHIHI YA KUBADILISHA MFUMO WA KIBADHIRIFU ULIOJIFICHA KWENYE POSHO ZISIZO ZA MSINGI NA KUBORESHA MASILAHI YA WATUMISHI WA UMMA KUPITIA MISHAHARA YAO.



MSIMAO WANGU

Kwanza najua na ninamini kuwa “ UMASIKINI SIO UZALENDO “ sipendi umasikini , nachukia umasikini lakini pia sipendi kuona mafanikio yangu yanabaki kwangu tu huku wengine wakiteseka , lakini siwezi pia kukumbatia umasikini kwa lengo lakuthibitisha uzalendo wangu .

Najua watu wa Jimbo langu wanataka maji , umeme na huduma bora za Afya na mambo mengi yenye sura hii lakini sitang’oa bomba la maji nyumbani kwangu kwa sababu jirani yangu hana maji ila nimtasaidia kwa kadri nitakavyoweza na yeye aepukane na adha hiyo ya ukosefu wa maji .

Najua shule za Kata hazina ufaulu mzuri na mazingira yake ni magumu , lakini sitampleka mtoto wangu kwenye shule zisizo na waalimu ili kuonyesha uzalendo bali nitapigania ubora wa shule hizo kuongezeka ili Wananchi wote wapate Elimu bora .

Zitto Julai 2012 stahili za Mbunge ziliongezwa kwa takribani shilingi milioni tatu ambazo ni sawa na milioni thelasini na sita kwa mwaka , je kwani Zitto hakugoma kupokea pesa hizo ili kuonyesha uzalendo wake ?

Zitto kuna wakati uliumwa ukapelekwa India kutibiwa , sasa kwani hukuwa mzalendo na kufanya mgomo ili utibiwe hapa Nchini ili kuonyesha Uzalendo wako ? na kuokoa pesa ya serikali kama ambavyo unaionea huruma kwenye posho ?

Zitto ningekuelewa , kama maisha unayoishi yangeendana na kauli zako za Kikomunisti lakini maisha yako na matendo yako na mienendo yako yanashindwa kutafsiri kauli zako .

MWISHO – MIMI SIAMINI KAMA MSINGI WA UZALENDO NI UMASIKINI . LAITI INGEKUWA HIVYO MAKUSUDI YA KUANZISHA MFUMO WA VYAMA VINGI ILI KUWAKOMBOA WATANZANI NA LINDI LA UMASIKINI ULIOSABABISHWA NA CCM YASINGEKUWA NA HAJA , NAJUA ASILIMIA 80 YA WATANZANIA NI MASIKINI SANA , JE WATANZANIA NI WAZALENDO KWA TAIFA LAO KULIKO WAMAREKANI ?


Namalizia kwa maneno ya Charles Darwin “ If the misery of the poor be caused not by the laws of nature, but by our institutions, great is our sin.”



Godbless J Lema
2/11/2013

No comments:

Post a Comment