Sakata la kujeruhiwa kwa Katibu wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, limepamba moto,
baada ya mkutano wa Waislamu jana kuibua mapya.
Kati ya mapya yaliyoibuliwa katika mkutano huo ni pamoja na kupitisha maazimio matatu likiwamo la kuhamasishana kutokipigia kura Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi utakaoitishwa wakati wowote kuanzia sasa.
Maazimio mengine yanawataka Waislamu kujiandaa kwa maandamano yatakayofanyika nchini kote kupinga dhuluma na kudai haki zao.
Pia kuitaka serikali iunde Tume huru ya uchunguzi wa tukio la kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda.
Maazimio hayo yalisomwa na Sheikh Kondo Juma Bungo, katika kongamano la waumini hao, lililoandaliwa na Jumuiya na Taasisi za KiislamuTanzania, katika viwanja vya Mwembeyanga, Temeke, jijini Dar es Salaam.
Akisoma maazimio hayo, Sheikh Kondo alisema tatizo la msingi dhidi ya Waislamu ni CCM.
Sheikh Kondo alisema juzi walishindwa kufanya maandamano kwa sababu hawakuwa wamejiandaa, hivyo anajiandaa kufanya maandamano nchini kote.
Hata hivyo, alisema Rais Jakaya Kikwete, bado ana nafasi ya kuundaTume huru kuchunguza tukio la
kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda na kwamba wakati hatua hiyo ikisubiriwa hatua nyingine zichukuliwe.
Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kushtakiwa mahakamani kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, Mkuu wa Kikosi cha Polisi kilichoongoza operesheni katika tukio lililosababisha kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda na askari polisi anayetuhumiwa kumpiga risasi Sheikh huyo.
Hatua nyingine ni kujiuzulu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Awali, akiwasilisha mada kuhusu yaliyosababisha Sheikh Ponda kujeruhiwa, Sheikh Suleiman Daudi, alisema kwenye kongamano hilo kuwa ni kuzungumzia madai ya Waislamu ya muda mrefu.
Alisema baadhi ya madai hayo ni Tanzania kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Nchi za Kiislamu (OIC) na kurejeshwa kwa Mahakamaya Kadhi.
Kwa mujibu wa Sheikh Suleiman, madai hayo yaliwahi kuwasilishwa na Waislamu kupitia halmashauri yao serikalini lakini hayakufanyiwa kazi.
Alisema wanashangazwa kuona baadhi ya makundi ya watu katika jamii, wakiwamo wanasiasa wakitoa kauli za uchochezi, kama vile nchi haitatawalika,lakini hawajawahi kufanyiwa kama alivyofanyiwa Sheikh Ponda.
Naye Sheikh Hussein Ismail, alisema Waislamu wanaviamini vyombo vya sheria nchini, hivyo akawataka Waislamu wachangie gharama za kuwezesha kusimamia kesi inayomkabili Sheikh Ponda mahakamani.
Kutokana na wito huo, Waislamu waliohudhuria kongamano hilo waliitikia na kuchangia fedha taslim katika viwanja hivyo.
No comments:
Post a Comment