Mosi, Serikali kutoa ahadi bila utekelezaji kwa miaka mingi. Mwaka 2012
na 2013 Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli amekuwa akirudia kauli
kwamba ujenzi wa Dar Es Salaam-Chalinze express road kuanza. Katika
mkutano wangu na wananchi jimboni tarehe 19 Januari 2014 kuhusu ujenzi
wa Barabara hiyo, nimesisitiza kwamba fedha za ujenzi wa barabara hiyo
hazijatengwa hivyo ujenzi hauwezi kuanza. Badala yake nilifafanua kwamba
Serikali inachokifanya kwa sasa ni kutafuta mkandarasi mwenye uwezo wa
kutafuta fedha na kujenga. Hivyo, ni muhimu Serikali ikawaeleza wananchi
ukweli na kuharakisha kutekeleza ahadi zilizotolewa kwa miaka mingi.
Pili; badala ya Serikali kuja na wazo la kujenga njia zaidi ya 6, ianze
kwanza kutekeleza ahadi ya njia hizo sita; kwa kuanza na ujenzi katika
umbali wa mita 60 zilizopo. Hivyo, sioni haja ya Serikali kujenga kwa
sasa mpaka eneo la upana wa mita 241 wakati ambapo kuna barabara
nyingine muhimu za pembezoni ya Barabara ya Morogoro ambazo
zikiharakishwa kujengwa zinaweza kupunguza foleni mf. Barabara ya
Goba-Mbezi-Msigani-Malambamawili-Kinyerezi na nyinginezo ambazo ujenzi
wake unasuasua.