UFAFANUZI KUHUSU UPANUZI NA MGOGORO KUHUSU UPANA WA BARABARA YA MOROGORO
Mosi, Serikali kutoa ahadi bila utekelezaji kwa miaka mingi. Mwaka 2012
na 2013 Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli amekuwa akirudia kauli
kwamba ujenzi wa Dar Es Salaam-Chalinze express road kuanza. Katika
mkutano wangu na wananchi jimboni tarehe 19 Januari 2014 kuhusu ujenzi
wa Barabara hiyo, nimesisitiza kwamba fedha za ujenzi wa barabara hiyo
hazijatengwa hivyo ujenzi hauwezi kuanza. Badala yake nilifafanua kwamba
Serikali inachokifanya kwa sasa ni kutafuta mkandarasi mwenye uwezo wa
kutafuta fedha na kujenga. Hivyo, ni muhimu Serikali ikawaeleza wananchi
ukweli na kuharakisha kutekeleza ahadi zilizotolewa kwa miaka mingi.
Pili; badala ya Serikali kuja na wazo la kujenga njia zaidi ya 6, ianze
kwanza kutekeleza ahadi ya njia hizo sita; kwa kuanza na ujenzi katika
umbali wa mita 60 zilizopo. Hivyo, sioni haja ya Serikali kujenga kwa
sasa mpaka eneo la upana wa mita 241 wakati ambapo kuna barabara
nyingine muhimu za pembezoni ya Barabara ya Morogoro ambazo
zikiharakishwa kujengwa zinaweza kupunguza foleni mf. Barabara ya
Goba-Mbezi-Msigani-Malambamawili-Kinyerezi na nyinginezo ambazo ujenzi
wake unasuasua. Tatu; Serikali kupotosha kwa miaka mingi
kuhusu upana wa barabara hiyo. Mwaka 2011, 2012 na 2013 Waziri wa Ujenzi
Dk John Magufuli amekuwa akidai kwamba upana wa barabara hiyo
unahusisha pia maeneo yenye upana wa mita 242 ( mita 121 kutoka katikati
ya barabara kwa kila upande) kuanzia Jimboni Ubungo hadi Kibaha; na
kwamba wananchi wanaoishi katika maeneo ya ndani ya upana huo ni
wavamizi wasiostahili kulipwa fidia. Kwa nyakati mbalimbali nimepinga
kauli hiyo ya Waziri na yamekuwepo malumbano kuhusu suala hilo. Mara
zote nimesisitiza kwamba upana wa barabara hiyo ni mita 60 (yaani 30 kwa
kila upande kutoka katika kati ya barabara). Hivyo, wakazi katika eneo
hilo hawajavamia barabara na wamehamia kihalali kwa msukumo wa Serikali
kuanzia wakati wa Operesheni vijiji ya mwaka 1970.
Mkutano
wangu na wananchi wa tarehe 19 Januari 2014 ulijadili suala hili
kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kupitia shauri Na 80
la 2005 na kutoa hukumu tarehe 31 Mei 2013 ambayo pamoja na mambo
mengine imetamka kuwa The Highway Ordinance Cap 167 Government Notice
No 161 of 5/5/1967 ambayo hutumiwa na Wizara ya Ujenzi na Tanroads
kuingia katika ardhi za wananchi “ni batili kwa kutofautiana na vifungu
vya 15 na 16 vya Sheria ya Ardhi ya Vijiji na 5 ya 1999”.
Tatu; kwa nyakati zote nimesisitiza kwamba iwapo Serikali inataka kutwaa
maeneo ya nyongeza kwa ajili ya ujenzi nje ya nafasi ambayo tayari
inawezesha ujenzi wa barabara hiyo basi Serikali ihakikishe inalipa
kwanza fidia kwa wananchi kabla ya kubomoa nyumba za wananchi na
kuwasababishia umaskini. Suala hili nalo nililisisitiza katika mkutano
wangu na wananchi tarehe 19 Januari 2014 katika eneo la Luguruni.
Hivyo, habari iliyoandikwa na Gazeti la Tanzania Daima 21 Januari 2014
(uk 2) kwamba Mnyika “alisema haoni ya kupanua barabara kutoka Kibaha
hadi Dar es Salaam wakati maeneo mengine ya nchi hayana barabara
zinazopitika kwa kirahisi” si sahihi.
Aidha, kauli ya Wakala wa
Barabara (TANROADS) kupitia Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar Es Salaam
Julius Ndyamkama kwamba “watu waliojenga kinyume cha sheria ndani ya
hifadhi ya barabara pembezoni mwa barabara ya Morogoro kuanzia Ubungo
hadi Kibaha wamekuwa wakidaganyana kuwa nyumba zinatakiwa kuwa umbali wa
mita 30 kutoka barabarani, lakini ukweli ni kwamba nyumba zinaruhusiwa
kujengwa umbali wa mita 121 kutoka katika barabara za TANROADS” nayo sio
sahihi.
Katika muktadha huo, namshauri Rais Jakaya Kikwete
kukaa na mawaziri wake kuwaelekeza kuipitia, kuiheshimu na kuwezesha
utekelezaji wa maamuzi ya mahakama pamoja na kuharakisha ujenzi wa
barabara huku ikilinda haki za msingi za wananchi wa majimbo ya Ubungo,
Kisarawe, Kibaha Mjini na Chalinze walioshi pembezoni mwa barabara hiyo
wenye haki zilizotambuliwa tangu wakati wa Operesheni Vijiji.
Kadhalika, badala ya kuendeleza malumbano Waziri wa Ujenzi Dk John
Magufuli na Watendaji wake wa Wakala wa Barabara (TANROADS) waelekeze
nguvu za haraka katika kusimamia ujenzi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa
Haraka (BRT) ambapo Mkandarasi (Starbag) na Wakala (DART) hawatekelezi
ipasavyo masharti ya mikataba.
Masharti hayo yanayokiukwa na
ni pamoja na kushindwa kuweka njia mbadala za kutosha na alama
inavyostahili na hivyo kusababisha msongamano mkubwa katika barabara ya
Morogoro wenye athari kwenye uchumi wa nchi na kuleta usumbufu kwa umma.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
21/01/2014
No comments:
Post a Comment