Sunday, May 11, 2014

JULIUS S. MTATIRO: VYAMA VIPYA VYA SIASA VINAWEZA KUWA NA MAANA KUBWA NA VINAWEZA KUWA HOVYO MNO

ALLAH Ibariki Nchi Yetu

VYAMA VIPYA VYA SIASA - MTIZAMO BINAFSI.
Vyama vipya vya siasa vinavyoanzishwa na kusajiliwa nchini Tanzania vinaweza kuwa na maana kubwa sana, na vinaweza kuwa hovyo mno.
Tayari tunajua kuna chama kikubwa hapa nchini na kinatumia kila mbinu NZURI na CHAFU kuendelea kuongoza nchi. Na kuna vyama vya upinzani vyenye ushawishi mkubwa lakin kutokana na sababu mbalimbali vyama hivyo havijaweza kupata ushindi mkubwa kwenye uchaguzi kwa miaka 20 sasa.
Vyama vya CUF, CHADEMA na NCCR vina ushawishi mkubwa sana hivi sasa, kila kimoja kikiwa na maeneo kadhaa makubwa ambayo kinaweza kushinda ikiwa vyama vingine vitakiunga mkono.
CCM imeendelea kushikilia maeneo makubwa zaidi na kushinda chaguzi mbalimbali kwa kutumia nafasi ya;
(1) kuwa na tume ya uchaguzi inayoteuliwa na CCM haohao,
(2) kuwa na uwezo mkubwa sana wa kifedha unaochota fedha kutoka serikalini, miradi ya chama ambayo wananchi waliporwa na kufanywa ya CCM, matajiri wengi wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kupata upendeleo wa shughuli zao, mataifa makubwa duniani yanayonufaika na mfumo wa CCM kuendelea kuwepo madarakani n.k.

(3) kuendelea kupata sapoti yote ya vyombo vya dola katika chaguzi ikiwemo wakuu wa mikoa, mawaziri, wakuu wa wilaya, wakuu wa polisi, polisi, mgambo, magereza n.k., hapa sijawaweka wakurugenzi wa halmashauri ambao moja kwa moja ndio pia wasimamizi wa uchaguzi,
(4) udhaifu wa vyama vya upinzani hasa pale ambapo vyama vyenyewe vinagombaniana kura galafu CCM wanapita kiulaini. Kwa mfano katika uchaguz wa kata 27 uliopita, CCM walishinda kata 23 na Upinzani 4. Lakini upinzani ulizikosa kata zaidi ya 11 kwa kugawana kura na kuiacha CCM ikipeta.
(5) raia kutokuwa na elimu ya uraia na ya kutambua kwa upana umuhimu wao katika masuala ya demokrasia na maendeleo. Wananchi wa Tanzania bado hawana elimu hii pana, wengi utawakuta wakisema "mambo ya kupiga kura yanawahusu wanasiasa" au utawasikia "hata tukichagua mwingine ni walewale tu, bora tuendelee na huyu".
(6) sababu nyingine mbalimbali mnazoweza kuzitaja hapa.
Lugha za namna hii za kukata tamaa huzikuti Kenya, Zambia, Afrika Kusini n.k. Huko wananchi wanajua turufu yao katika kuchagua viongozi waadilifu na wenye kiu na maendeleo ya wananchi.
Hapa kwetu raia anauza shahada yake ya kupigia kura kwa kilo ya sukari au kipande cha khanga, tena utamkuta anajitapa kuwa yeye uchaguzi umemnufaisha na anawacheka wale waliokataa kilo ya sukari.
Pamoja na mazingira yote hayo, vyama vinapaswa kuendelea kujipanga na kuchukua hatua.
Kama vyama vya upinzani vya muda mrefu vina changamoto kubwa namna hii, ni ukweli ulio wazi kuwa vyama vipya vina changamoto kubwa zaidi. Changamoto hizi kwa wote zina maana kuwa kazi mbele ya safari bado ni kubwa mno.
Vyama vipya vinaweza kutumia fursa nzuri ya kusoma makosa ya vyama vilivyopo na kuanzisha utaratibu mzuri sana kujitofautisha na mifumo iliyopo katika vyama vikongwe. Namna hii vitaweza kufanikiwa kuja kuwa na nguvu siku za usoni, japokuwa wakati mwingine wananchi hawajui tofauti ya mifumo iliyoko katika vyama na kwamba unaweza kuja na kitu kipya kabisa na wakakuona huna maana na ni sawa tu na aliyepo.
Kwa mfano, ukija na siasa za kutumia Bajaji ili kubana matumizi wananchi wengi wasio na elimu ya uraia watasema huyu ni masikini kama sisi, hana uwezo wa kubadilisha maisha yetu. Unaweza kuja na maVX makubwa kabisa na wananchi wakasema huyu naye amekuja kula kama aliyepo, ni bora tuendelee kumchagua tuliyemzoea. IT IS VERY TRICKY!!!
Lakini ikiwa vyama vipya vinavyoanzishwa vinakuja kuvipinga vilivyopo huku kwa SIRI vikiiunga mkono CCM na hata kupokea misaada ya kujijenga kutoka CCM, vitakuwa ni hovyo na vya AJABU KABISA. CCM hadi sasa imeanzisha utitiri wa vyama, vinaunga mkono almost kila kinachosemwa na CCM. Ni vyama maslahi na vyama MATUMBO. Namuomba sana mungu, hivi vyama vinavosajiliwa hivi sasa visiwe vimeanzishwa na mkono wa CCM, viwe vyama mbadala na siyo matawi ya CCM.
Ikiwa vyama hivi vipya vitajinyumbua na kuonesha uwezo na upeo wake katika kutetea wananchi na maisha yao, na ikiwa vitapinga kila baya linalofanywa na chama au mtu yeyote kwa maslahi ya wananchi, vitakuwa vyama bora na polepole wananchi watavielewa.
Vyama hivi vichague, au kujiunga na LUNDO la tu-vyama tudogo tudogo tulivojazana na "hata akaunti ta benki hatuna", au kujiunga na watanzania wanaoendelea kusaka mbadala wa CCM. Natumai CHAGUO la pili ni sahihi sana kwao.
Mungu Ibariki Tanzania.

No comments:

Post a Comment