MJADALA wa Bunge Maalum la Katiba, hasa kuhusu muundo wa Muungano
bado unavuta hisia za wengi kutokana na yanayozungumzwa.
Tunapoadhimisha miaka 50
ya Muungano huo, mambo mengi yanazidi kuelezwa, japo siyo mapya kwa vile
yamekwishawahi kuelezwa katika Tume mbalimbali huko nyuma kama ya Jaji Robert
Kisanga, Jaji Francis Nyalali na Jaji Joseph Warioba.
Mzee Warioba pia katika
Tume ya Marekebisho ya Katiba aliwasilisha maoni kama yale yale, na safari hii
yakiwa yametolewa mapendekezo lukuki ambayo kwayo ndiyo yaliyozaa mjadala
mkubwa ndani ya Bunge Maalum.
Kubwa lililojitokeza ni
kwa Wajumbe wengi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutamka hadharani kwamba wao
wanataka muundo wa Muungano wa Serikali Mbili na siyo Tatu kama
ilivyopendekezwa na Tume ya Warioba.
Wengi wao wamekejeli
hata takwimu zilizotumiwa na Tume hiyo kwamba siyo sahihi na hazibebi mawazo ya
Watanzania wote ambao kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka
2012 wamefikia milioni 44.
Kila anayesimama kupinga
takwimu hizo, anasema ‘yeye amezungumza na wananchi anaowawakilisha, ambao
wanataka serikali mbili’. Kati ya hao, hajaonekana hata mtu mmoja aliyethubutu,
japo kwa bahati mbaya, naye kutoa takwimu zake kwamba watu anaowazungumzia ni
wangapi na alifanya ama kukusanya wapi takwimu hizo na kwa utaratibu upi.
Badala yake
kinachoonekana katika Bunge hilo Maalum ni hoja za nguvu, ambazo kwa namna moja
ama nyingine, ndizo zilizowafanya Wajumbe wanaounda kundi la UKAWA wakaamua
kususia vikao hivyo kwa maelezo kwamba CCM ‘imepora rasimu’ na inataka matakwa
yake ndiyo yasikilizwe.
Wimbi kubwa la kuhusu
muundo wa Muungano lilipotokea mwaka 1993 baada ya aliyekuwa Mbunge wa Chunya
wakati huo, Njelu Kasaka, kutoa hoja binafsi ya kutaka Serikali ya Tanganyika
ndani ya Muungano, mambo mengi yalisemwa.
CCM ilibaini kwamba
nguvu za wabunge waliokuwa wanaunda Kundi la G55 (baadaye likawa G65) zilikuwa
kubwa ikatambua kwamba Muungano ulikuwa mashakani.
Ndiyo maana mwaka 1994
CCM ikaendesha kura ya maoni kwa wanachama wake – siyo Watanzania takriban
milioni 30 wa wakati huo – ili kupata msimamo wa muundo wa serikali.
Wakati huo wapo
waliotaka iwepo Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, hivyo ziwepo serikali
tatu. Wapo waliotaka ziendelee kubaki serikali mbili, lakini pia walikuwepo
waliotaka ibaki serikali moja tu. Hoja zilikuwa nzito na zilihusisha maslahi ya
Watanzania wote.
Waliokuwa wakitetea
Muungano ilionekana waliutetea kwa lugha kali ya hasira, ghadhabu na hata
vitisho vya kuwafukuza wenzao kwenye Chama. Waliodai Utanganyika nao walidai
kwa lugha hiyo hiyo ya ukali, wakijibu mapigo.
Wakati huo CCM ilikuwa
na wanachama 3,506,355, lakini walioulizwa kwenye Kura ya Maoni
walikuwa 1,349,501 tu, sawa na asilimia 33.49 ya wanachama wote nchi
nzima.
Wanachana 833,317 ambao
ni asilimia 61.75 ya wanachama 1,349,501 waliopiga kura walipendekea serikali
mbili, wanachama 394,189 sawa na asilimia 29.21 walipendekeza serikali moja, na
wanachama 111,604 ambao ni asilimia 8.27 walitaka serikali ya Tanganyika ndani
ya Muungano. Kura za maoni zilizoharibika zilikuwa asilimia 0.67 ambazo ni za
wanachama 9,042.
Tulielezwa baada ya kura
hizo za maoni, ambazo hatujui kulikuwa na uwazi kiasi gani, kwamba Serikali ya
Chama cha Mapinduzi imekubaliana kwamba muundo wa Muungano uendelee ule ule wa
serikali mbili, lakini wakielekea kwenye serikali moja! Narudia - Serikali
Moja!
Hakuna anayejua kama
kura hizo zilikuwa sahihi au la, kwa sababu walioitisha ni wanaCCM wenyewe,
waliozisimamia ni viongozi wa CCM, waliohesabu ni hao hao, na waliotangaza ni
wenyewe!
Nakumbuka aliyekuwa Mkuu
wa Mkoa wa Mara wakati huo, Joseph Butiku alikaririwa Jumanne, Agosti 23, 1994
kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam wakati akishiriki mjadala wa hoja ya
serikali ya kufuta Azimio la Bunge la mwaka 1993 la kuanzishwa kwa serikali ya
Tanganyika ndani ya Muungano na kusema Chama kilikuwa kimeamua kuendelea na
serikali mbili.
"... Huu ndio
msimamo wa Chama; serikali mbili kuelekea serikali moja na kama Waziri Mkuu
hataki, shauri yake, kama Rais wa Zanzibar hataki, shauri yake, maana Chama cha
Mapinduzi kina utaratibu wa kuliongoza taifa hili..." alinukuliwa akisema.
Jambao ambalo CCM
walilisahau, na ambalo wanaendelea kutolitambua ni kwamba, suala hili ni nyeti
na linawagusa wote, wananchi wa Tanzania kwa ujumla wao, bila kujali itikadi
zao za siasa.
Kusema kwamba wanaCCM
Tanzania wanataka serikali mbili halafu kuchukulia kama ndio uamuzi wa
Watanzania wote ni makosa na kinyume na demokrasia, kwa sababu kama mwaka 1994
wanachama wake hawakufika hata milioni 4, itakuwaje kwa sasa ambapo tayari kuna
vyama vingi?
Kama wanapinga takwimu
za Warioba ambazo zinawakilisha maoni ya wengine yaliyochukuliwa katika
utaratibu unaojulikana kisheria, kwa nini Watanzania waamini takwimu zao ambazo
zimetolewa kwa maslahi ya chama?
Sasa kilichotokea wakati
ule mwaka 1994 ndicho kinachoonekana katika Bunge Maalum la Katiba ambalo
linatarajiwa kuahirishwa Ijumaa ya tarehe 25 Aprili 2014 kupisha Bunge la
Bajeti.
Kuna haja ya kutafakari.
Sisi sote ni Watanzania na tuipiganie nchi yetu kwa pamoja, tusitangulize mbele
maslahi binafsi.
Huu ni mtazamo wangu, na
kumbukumbu zangu, nijibuni kwa hoja.
Nawasilisha.
Ndugu yenu,
Daniel Mbega
Iringa, Tanzania
0656 331974
No comments:
Post a Comment