Tuesday, July 16, 2013

WAISLAM WAASWA KULIOMBEA TAIFA KATIKA KIPINDI HIKI CHA RAMADHAN

Waumini wa dini ya Kislamu wakiswali
Waislamu nchini wametakiwa kutumia kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan kuliombea Taifa liepukane na majanga na migogoro mbalimbali, ikiwamo ya kidini na kisiasa liwe la amani na utulivu.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Hajji Kavan, Muhammad Jaffa Pirali, alisema hayo alipongumza na waandishi wa habari katika mashindano ya usomaji wa Qur’an, yaliyofanyika katika viwanja vya Mwembe Yanga, jijini Dr es Salaam.

Alisema Tanzania ni nchi ya amani na utulivu hivyo kuna haja ya kuiombea iendelee.

“Waislamu wengi tunaamini huu ni mwezi wenye neema na baraka kubwa, hivyo tunaweza hata kuutumia kwa kufanya maombi ya kudumisha amani na utulivu nchini kwetu ingawa maombi yanaweza kufanyika siku zote hata kama siyo mwezi wa Ramadhani” alisema Pirali.

Alisema katika siku za karibuni kumetokea migogoro na matukio mbalimbali nchini hali iliyosababisha kuonekana Tanzania haina amani, lakini kwa kudra za Mwenyezi Mungu matatizo hayo yanaweza yasijitokeze tena.

Aliwataka wanaofanya vitendo vya uchochezi kwa maslahi yao binafsi kwa kuwafanya Waislamu kuingia katika migogoro ya kidini na madhehebu mengine kuachana na tabia hiyo kwa kuwa vinapelekea madhara makubwa kwa Taifa.

“Waislamu tunapenda amani na hakuna sehemu yoyote katika Qur’an inavyowataka Waislamu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani, hivyo tuipukane na wachochezi wanaotaka kutuingiza katika migogoro

130 WAUAWA KATIKA MAPIGANO MASHARIKI MWA DRC



Mapigano makali yaliyojiri kati ya majeshi ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa kundi la M23 katika kipindi cha masaa 48 yaliyopita, yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 130 karibu na mji wa Goma, ulioko katika jimbo la Kivu Kaskazini.
Hayo yamesemwa na Lambert  Mende Omalanga Waziri wa Habari na msemaji wa serikali ya Kongo wakati alipozungumza na waandishi wa habari mjini Kinshasa. Omalanga ameongeza kuwa, mapigano makali yalishuhudiwa katika eneo la Mutaho lililoko umbali wa kilomita 7 kaskazini mwa Goma kati ya vikosi vya jeshi la serikali na waasi na M23, na kwamba hatimaye vikosi vya serikali ya Kinshasa vimefanikiwa kuwaangamiza waasi 120, kuwatia mbaroni waasi 12 na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Omalanga ameongeza kuwa, wanajeshi 10 wa serikali pia waliuawa. Inafaa kuashiria hapa kuwa, mwezi Novemba mwaka jana, kundi la waasi wa M23 lilifanikiwa kuuteka mji wa Goma na kuukalia kwa mbavu kwa muda wa siku 10, lakini lililazimika  kuondoka baada ya kukabiliwa na mashinikizo makubwa ya nchi za eneo la Ukanda wa Maziwa Makuu ya Afrika.

Monday, July 15, 2013

CHADEMA CHASHINDA VITI VYA UDIWANI ARUSHA

Chadema kimethibitisha umwamba wake katika siasa za Jimbo la Arusha Mjini, baada ya kutetea kwa kishindo kata zake nne kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika jana.
Katika uchaguzi huo uliokuwa unasubiriwa kwa hamu na ambao ulichukuliwa kama kipimo cha siasa za Arusha ambazo zimekuwa na mvutano mkubwa, Chadema kiliongoza katikia vituo vyote 136 vya kupigia kura Kata za Elerai, Kaloleni, Kimandolu na Themi.
Kata hizo zilikuwa wazi tangu mwaka 2011 baada ya Chadema kuwatimua wanachama wake waliokuwa madiwani Estomih Mallah(Kimandolu), John Bayo (Elerai), Reuben Ngowi (Themi) na Charles Mpanda (Kaloleni).
Matokeo
Katika matokeo yaliyotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi Kata ya Elerai, Obedi Meng’oriki mshindi alikuwa Jeremiah Mpinga wa Chadema aliyepata kura 2,047 dhidi ya 1,471 za Emmanuel Laizer wa CCM. Katika Kata hiyo kulikuwa na wagombea wengine ambao ni John Bayo (CUF; kura 302), Seif Shimba (CCK; kura 3) na Boisafi Shirima (TLP;1).
Katika Kata ya Themi, Kinabo Edmund wa Chadema aliibuka na ushindi baada ya kupata kura kupata kura 674. Msimamizi wa Uchaguzi Kata hiyo, Ezeka Mboya alisema Kinabo alifuatiwa na Victor Mkolwe aliyepata kura 326 na Lobora Ndarpoi wa CUF alipata kura 307.
Kata ya Kaloleni, Msimamizi wa Uchaguzi, Anna Ledisa alimtangaza Kessi Lewi wa Chadema kuwa mshindi kwa kura 1,470 dhidi ya Emmanuel Mliari wa CCM aliyepata kura 330 na Abbas Mkindi wa CUF aliyepata kura 275 na Ngilishi Pauli wa Demokrasia Makini aliyeambulia kura mbili.
Kata ya Kimandolu, Msimamizi wa Uchaguzi, Suleiman Kilingo alimtangaza Mchungaji Rayson Ngowi wa Chadema kuwa mshindi kwa kura 2,761 na kumshinda Edna Saul wa CCM aliyepata kura 1,163. Kwa matokeo hayo, Chadema sasa kimefikisha madiwani 12 wakati CCM kimebakiwa na kumi na moja na TLP kina wawili.
Ushindi huo wa Chadema una athari kwa nafasi ya Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo kwani CCM kina wajumbe 14 tu kwenye Baraza la Madiwani, TLP wawili wakati Chadema sasa kimefikisha 15. Wabunge wa majimbo na wale wa viti maalumu pia ni madiwani.
Aidha, Chadema kina nafasi ya kuongeza kiti kingine cha udiwani kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kinatarajiwa kuitisha uchaguzi mdogo Kata ya Sombetini.
Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba alimwambia mwandishi wetu kuwa tume yake inatarajia kuitisha uchaguzi mdogo hivi karibuni baada ya kata hiyo kutangazwa wazi na Ofisi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi.
Malaba alisema uchaguzi huo utaitishwa baada ya aliyekuwa Diwani wake, Alphonce Mawazo kujitoa CCM na kujiunga na Chadema hali inayokifanya chama tawala kuwa katika wakati mgumu kukitetea kiti hicho.

Monday, July 8, 2013

WATU 53 WAMEUAWA KATIKA MASHAMBULIZI YA KIJESHI NCHINI MISRY


Haya yanajiri huku ghasia zikiendelea baada ya kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa rais Mohammed Morsi
Chama cha Brotherhood kimwarifu kuwa watu 53 wameuawa na wengine zaidi ya 500 wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi mjini Cairo nje ya kambi ya jeshi la nchi hiyo.


Habari zinadai kuwa watu hao ni wafuasi wa Rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Morsi waliokua wamekusanyika nje ya kambi hiyo ya jeshi wakipinga kuondolewa madarakani kwa rais Morsi.

Wizara ya Afya ya Misri imetaja idadi ya waliouawa kwenye mashambulizi hayo ya jeshi ya leo kuwa watu 40. Watu walioshuhudia wameeleza kuwa jeshi la Misri limetumia silaha hai kuwatawanya wafuasi wa Muhammad Morsi huko katika mji wa Nasr mashariki mwa Cairo. 

Kundi la Muslima Brotherhood limewataka raia wa Misri kuwapinga wale linawaita wanaopokonya raia uhuru na demokrasia. 
Brotherhood imelaumu jeshi kwa kuwaua raia wake.
Katika kikao na waandishi wa habari, wafuasi hao walimlaani vikali mkuu wa jeshi Abdel Fattah Al-Sisi na kumtaja kama muuaji aliyewashambulia raia wenzake.
Waandamanaji hao wanasema vikosi maalum viliwafyatua risasi baada ya swala ya fajir huku wengine wakishambuliwa walipokusanyika nje ya makao ambako bwana Morsi anadhaniwa kuzuiliwa wakitaka watawala kumwachilia huru.

Chama cha Brotherhood  kinasema kuwa  wafuasi wake wameuawa wakati jeshi la Misri lilipoushambulia umati wa watu hao waliokuwa wameketi chini nje ya kambi zao wakipinga kitendo cha kupinduliwa Rais Muhammad Morsi.