Mwelekeo wa Taifa la Tanzania utaanza kujulikana
leo mchana Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakapozindua rasimu ya Katiba
Mpya kwenye tukio la kihistoria litakalofanyika kwenye Viwanja vya
Karimjee, Dar es Salaam.
Watanzania wanasubiri kwa hamu kuona kama rasimu
hiyo itakuja na majibu ya maswali magumu, makubwa ya muundo wa Muungano,
madaraka ya Rais, uteuzi wa mawaziri kutokana na wabunge, muundo wa
wakuu wa mikoa/wilaya na muundo wa mihimili mingine miwili ya dola;
Mahakama na Bunge.
Uzinduzi wa rasimu hiyo unafanyika baada ya Tume
hiyo kufanyia kazi ya uchambuzi wa maoni ya wananchi. Maoni hayo
yalitolewa na wananchi wapatao 1,015,564 kwa njia mbalimbali ikiwa ni
pamoja na waliohudhuria mikutano ya moja kwa moja, waliotuma ujumbe
mfupi wa simu (sms), barua pepe na kutumia mitandao ya kijamii.
Idadi ya makundi yaliyotoa maoni ni 170 zikiwamo
asasi 22 za dini, kiraia 72, taasisi za Serikali 71, vyama vya siasa 19,
viongozi na watu mashuhuri 43 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Rasimu hiyo ndiyo itakayopelekwa kwenye Mabaraza
ya Katiba na itajadiliwa miezi mitatu ili kuona kama mapendekezo ya Tume
hiyo baada ya kuchambua maoni hayo ya wananchi yanafaa au yanahitaji
marekebisho.
Huo ni mwendelezo wa mchakato wa mabadiliko ya
Katiba ulioanza mwaka jana baada ya Rais Jakaya Kikwete kuteua wajumbe
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuanza kukusanya maoni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam
jana na Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid uzinduzi huo utaonyeshwa moja
kwa moja kupitia Televisheni ya Taifa (TBC) kuanzia saa nane mchana.
Taarifa hiyo iliwaomba wananchi kufuatilia
uzinduzi huo kwa umakini ili waweze kujua kinachoendelea. Kuzinduliwa
kwa rasimu hiyo kutaanzisha upya mjadala wa Katiba ambayo inatungwa kwa
mara ya sita.
Katiba iliwahi kutengenezwa mwaka 1961 wakati
Tanganyika ilipopata Uhuru, mwaka 1962 baada ya nchi kuwa Jamhuri, mwaka
1964 ilipoundwa Katiba ya Muda baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana
na mwaka 1965 ilitungwa Katika Mpya iliyodumu hadi mwaka 1977 baada ya
vyama vya Tanu na ASP kuungana na kuifanya nchi kuwa chini ya utawala wa
chama kimoja cha siasa.
Kwa upande wa Zanzibar kumekuwapo Katiba Tatu.
Kwanza ni ile ya Uhuru iliyotungwa mwaka 1963, Mwaka 1979 ikatungwa
Katiba nyingine na ya mwisho ni ile ya mwaka 1984.
Muundo wa Muungano
Kwa muda mrefu, suala la muundo wa Serikali mbili katika Muungano limekuwa mwiba katika siasa za Tanzania Bara na Zanzibar.
CHANZO: MWANANCHI