Friday, April 25, 2014

NAIKUMBUKA KURA YA MAONI YA CCM YA MWAKA 1994 KUHUSU MUUNGANO

MJADALA wa Bunge Maalum la Katiba, hasa kuhusu muundo wa Muungano bado unavuta hisia za wengi kutokana na yanayozungumzwa.
Tunapoadhimisha miaka 50 ya Muungano huo, mambo mengi yanazidi kuelezwa, japo siyo mapya kwa vile yamekwishawahi kuelezwa katika Tume mbalimbali huko nyuma kama ya Jaji Robert Kisanga, Jaji Francis Nyalali na Jaji Joseph Warioba.

Mzee Warioba pia katika Tume ya Marekebisho ya Katiba aliwasilisha maoni kama yale yale, na safari hii yakiwa yametolewa mapendekezo lukuki ambayo kwayo ndiyo yaliyozaa mjadala mkubwa ndani ya Bunge Maalum.

Kubwa lililojitokeza ni kwa Wajumbe wengi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutamka hadharani kwamba wao wanataka muundo wa Muungano wa Serikali Mbili na siyo Tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Warioba.
Wengi wao wamekejeli hata takwimu zilizotumiwa na Tume hiyo kwamba siyo sahihi na hazibebi mawazo ya Watanzania wote ambao kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 wamefikia milioni 44.
Kila anayesimama kupinga takwimu hizo, anasema ‘yeye amezungumza na wananchi anaowawakilisha, ambao wanataka serikali mbili’. Kati ya hao, hajaonekana hata mtu mmoja aliyethubutu, japo kwa bahati mbaya, naye kutoa takwimu zake kwamba watu anaowazungumzia ni wangapi na alifanya ama kukusanya wapi takwimu hizo na kwa utaratibu upi.

Badala yake kinachoonekana katika Bunge hilo Maalum ni hoja za nguvu, ambazo kwa namna moja ama nyingine, ndizo zilizowafanya Wajumbe wanaounda kundi la UKAWA wakaamua kususia vikao hivyo kwa maelezo kwamba CCM ‘imepora rasimu’ na inataka matakwa yake ndiyo yasikilizwe.

Wimbi kubwa la kuhusu muundo wa Muungano lilipotokea mwaka 1993 baada ya aliyekuwa Mbunge wa Chunya wakati huo, Njelu Kasaka, kutoa hoja binafsi ya kutaka Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, mambo mengi yalisemwa.

CCM ilibaini kwamba nguvu za wabunge waliokuwa wanaunda Kundi la G55 (baadaye likawa G65) zilikuwa kubwa ikatambua kwamba Muungano ulikuwa mashakani.
Ndiyo maana mwaka 1994 CCM ikaendesha kura ya maoni kwa wanachama wake – siyo Watanzania takriban milioni 30 wa wakati huo – ili kupata msimamo wa muundo wa serikali.
Wakati huo wapo waliotaka iwepo Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, hivyo ziwepo serikali tatu. Wapo waliotaka ziendelee kubaki serikali mbili, lakini pia walikuwepo waliotaka ibaki serikali moja tu. Hoja zilikuwa nzito na zilihusisha maslahi ya Watanzania wote.

Waliokuwa wakitetea Muungano ilionekana waliutetea kwa lugha kali ya hasira, ghadhabu na hata vitisho vya kuwafukuza wenzao kwenye Chama. Waliodai Utanganyika nao walidai kwa lugha hiyo hiyo ya ukali, wakijibu mapigo.

Wakati huo CCM ilikuwa na wanachama 3,506,355, lakini walioulizwa kwenye Kura ya Maoni walikuwa 1,349,501 tu, sawa na asilimia 33.49 ya wanachama wote nchi nzima.
Wanachana 833,317 ambao ni asilimia 61.75 ya wanachama 1,349,501 waliopiga kura walipendekea serikali mbili, wanachama 394,189 sawa na asilimia 29.21 walipendekeza serikali moja, na wanachama 111,604 ambao ni asilimia 8.27 walitaka serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano. Kura za maoni zilizoharibika zilikuwa asilimia 0.67 ambazo ni za wanachama 9,042.
Tulielezwa baada ya kura hizo za maoni, ambazo hatujui kulikuwa na uwazi kiasi gani, kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekubaliana kwamba muundo wa Muungano uendelee ule ule wa serikali mbili, lakini wakielekea kwenye serikali moja! Narudia - Serikali Moja!
Hakuna anayejua kama kura hizo zilikuwa sahihi au la, kwa sababu walioitisha ni wanaCCM wenyewe, waliozisimamia ni viongozi wa CCM, waliohesabu ni hao hao, na waliotangaza ni wenyewe!

Nakumbuka aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara wakati huo, Joseph Butiku alikaririwa Jumanne, Agosti 23, 1994 kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam wakati akishiriki mjadala wa hoja ya serikali ya kufuta Azimio la Bunge la mwaka 1993 la kuanzishwa kwa serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano na kusema Chama kilikuwa kimeamua kuendelea na serikali mbili.
"... Huu ndio msimamo wa Chama; serikali mbili kuelekea serikali moja na kama Waziri Mkuu hataki, shauri yake, kama Rais wa Zanzibar hataki, shauri yake, maana Chama cha Mapinduzi kina utaratibu wa kuliongoza taifa hili..." alinukuliwa akisema.
Jambao ambalo CCM walilisahau, na ambalo wanaendelea kutolitambua ni kwamba, suala hili ni nyeti na linawagusa wote, wananchi wa Tanzania kwa ujumla wao, bila kujali itikadi zao za siasa.

Kusema kwamba wanaCCM Tanzania wanataka serikali mbili halafu kuchukulia kama ndio uamuzi wa Watanzania wote ni makosa na kinyume na demokrasia, kwa sababu kama mwaka 1994 wanachama wake hawakufika hata milioni 4, itakuwaje kwa sasa ambapo tayari kuna vyama vingi?

Kama wanapinga takwimu za Warioba ambazo zinawakilisha maoni ya wengine yaliyochukuliwa katika utaratibu unaojulikana kisheria, kwa nini Watanzania waamini takwimu zao ambazo zimetolewa kwa maslahi ya chama?
Sasa kilichotokea wakati ule mwaka 1994 ndicho kinachoonekana katika Bunge Maalum la Katiba ambalo linatarajiwa kuahirishwa Ijumaa ya tarehe 25 Aprili 2014 kupisha Bunge la Bajeti.
Kuna haja ya kutafakari. Sisi sote ni Watanzania na tuipiganie nchi yetu kwa pamoja, tusitangulize mbele maslahi binafsi.
Huu ni mtazamo wangu, na kumbukumbu zangu, nijibuni kwa hoja.
Nawasilisha.

Ndugu yenu,
Daniel Mbega
Iringa, Tanzania
0656 331974

No comments:

Post a Comment